Habari Mseto

Yaibuka demokrasia ndani ya ODM imekuwa ndoto

October 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

BAADHI ya wanachama wa ODM wamekashifu viongozi wa kitaifa wa chama hicho kwa kuangamiza demokrasia kwa uamuzi wao wa kutoandaa uchaguzi wa viongozi wa matawi.

ODM ilitangaza kwamba hakitaandaa uchaguzi bali kitajaza nafasi zilizoachwa wazi na waliokufa au kuhama chama hicho bila uchaguzi.

Katika Kaunti ya Kisii, viongozi wa vijana wa chama hicho walisema tangazo hilo la viongozi wa kitaifa kwamba uchaguzi hautafanyika kwa sababu ya janga la corona ni kinyume na katiba ya ODM na maono ya demokrasia.

Viongozi hao wamewataka maafisa wa kitaifa kubadilisha msimamo huo.Mwenyekiti wa vijana wa ODM eneo la Kitutu chache Kaskazini, Bw Steve Junior na mwenzake wa Nyaribari, Bi Jerusha Mogaka, pamoja na wajumbe walisema wanawazia kuchukua hatua za kisheria kupinga uamuzi wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC).

“Kuandaa uchaguzi ni haki inayotambuliwa na katiba ya Kenya na ile ya chama cha ODM. Itakuwa makosa kudumisha hali ilivyo kwa sababu inakiuka katiba hizi mbili. Kuna watu ambao wamehudumu, kwa mfano, kama viongozi wa vijana na wamepita miaka 35. Watawezaje kuwakilisha vijana ilhali umri wao umepita wa vijana? Hii pia inakiuka kanuni za Umoja wa Mataifa,” alisema Bw Junior.

Jana, baadhi ya wabunge wa ODM walioomba tusitaje majina yao pia walikosoa uamuzi wa chama kutofanya uchaguzi wakisema sio wa kidemokrasia.

Walisema hatua hiyo itawapatia maafisa ambao sio maarufu mashinani fursa ya kuendelea kuhudumu licha ya kuwa hawawezi kuvutia wafuasi zaidi chamani.

“Ninahisi baraza la kitaifa la wajumbe lingepatiwa nafasi ya kufanya uamuzi kuhusu uchaguzi badala ya maafisa wakuu kutulazimishia hatua hii,” alisema mbunge mmoja kutoka Nyanza.

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi alisema Bodi ya kitaifa ya uchaguzi ya chama hicho, itapatiwa jukumu la kujaza nafasi zilizo wazi kuanzia vituo vya kupigia kura na wadi.

“Ofisi itasimamia shughuli ya kujaza nafasi hizo katika matawi ambayo ni maeneobunge na kamati shirikishi za kaunti,” aliongeza Bw Mbadi.

Alisema kwamba mfumo huo utatumiwa hadi NEB itoe ratiba ya shughuli hiyo inayotarajiwa kufanyika kati ya Oktoba na Desemba.

Msajili wa vyama vya kisiasa Ann Nderitu alipoulizwa kuhusu hatua ya ODM ya kuteua wanachama wa kujaza nafasi tofauti badala ya kufanya uchaguzi, alisema anaweza kutoa kauli yake baada ya chama hicho kumfahamisha rasmi kuhusu suala hilo.

“ODM haijatuandikia rasmi kuhusu mipango ya kujaza nafasi zilizo wazi badala ya kufanya uchaguzi ingawa tarehe yao ya kufanya uchaguzi haijafika,” alisema.

“Watakapotuandikia, tutawashauri ipasavyo. Kinachoripotiwa na kilichoandikwa vinaweza kuwa tofauti na ndio sababu tutasubiri watuandikie rasmi,” alisema Bi Nderitu.