Askofu amtaka Uhuru apige marufuku kampeni za 2022
Na SHABAN MAKOKHA
ASKOFU Jackson Ole Sapit wa Kanisa la Kianglikana Kenya (ACK), anamtaka Rais Uhuru Kenyatta kupiga marufuku kampeni zote za uchaguzi wa 2022 na badala yake kuwaagiza viongozi wote kuwahudumia Wakenya.
Bw Sapit alisema kuwa viongozi wa Serikali na Upinzani wanapaswa kuwadhibiti wanachama wao ambao wanaendelea kujihusisha kwenye kampeni za mapema.
Alieleza viongozi hao wanapaswa kuelekeza juhudi zao kwenye mikakati itakayoboresha maisha ya Wakenya, kama uendelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aliwarai viongozi kutambua haja ya kuielekeza nchi kwenye njia inayofaa, badala ya sasa, ambapo majibizano makali baina ya wanasiasa yanatishia umoja na uthabiti uliopo.
Akihutubu jana katika Kanisa la St Luke’s ACK Cathedral, Butere, Kaunti ya Kakamega, Bw Sapit alisema kuwa majibizano hayo ni hatari kwa nchi.
“Tunawaomba viongozi kwenye Serikali na katika Upinzani kuwa waangalifu wanapozungumza katika mikutano ya umma, hasa wanapowahutubia wafuasi wao. Inasikitisha kuwa baadhi ya semi wanazotoa zinaweza kuwachochea Wakenya ama kuzua rabsha zisizofaa,” akasema.
Alieleza kuna haja viongozi wote nchini kufanya kikao cha pamoja kudhibiti hali hiyo, hadi pale Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itakapowaruhusu kufanya kampeni.Alieleza sikitiko lake kuwa wanasiasa nchini huendesha mikutano yao kama kila siku ni wakati wa kampeni. Alilalamika wengi huwa hawatilii maanani masuala muhimu ambayo yanamfaidi mwananchi.
“Wakati wa kampeni haujafika kwani imebaki miaka miwili. Viongozi wanapaswa kusimamisha siasa kwa sasa na kuangazia maendeleo. Si vyema wananchi kushuhudia siasa za majibizano kila wakati bila kutoa nafasi kwa utekelezaji wa masuala muhimu yanayowafaa,” akasema.
Alieleza kuwa mwelekeo wa siasa nchini kwa sasa umekitwa kwa lengo la kuwagawanya Wakenya kwenye misingi ya kitabaka.Hivyo, aliwaomba viongozi kukoma kuelekezeana matusi na badala yake kuanzisha miradi itakayowafaidi wananchi kwa muda mrefu.
Bw Sapit alieleza hofu yake kwamba vijana wengi nchini hawana ajira, ila viongozi wanaangazia siasa za 2022, badala ya kusuluhisha tatizo hilo.
“Vijana wanapaswa kupewa ajira, kwani nafasi za kufanya biashara ni chache. Janga la virusi vya corona limetuathiri vibaya, hasa uchumi wa nchi. Haya ndiyo masuala tunayopaswa kuangazia,” akasema.
Alisema mikakati ya kukabiliana na janga hilo na kubuni nafasi kwa vijana ndiyo inapaswa kupewa kipaumbele.Bw Sapit, ambaye ametangaza kuunga mkono Mpango wa Maridhiano (BBI), alisema kuwa tangu handisheki kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, mazingira ya siasa yalibadilika nchini huku miradi muhimu ikipuuziliwa mbali.
Alisema ripoti ya BBI inawapa Wakenya matumaini mapya kwani inataja masuala ambayo lazima yashughulikiwe kwa dharura ili kuleta utangamano zaidi nchini.