Joho atenga Sh30 milioni kumaliza kunguru wanaohangaisha watalii

Na WINNIE ATIENO

SERIKALI ya Gavana Ali Hassan Joho inapanga kutenga Sh30 milioni ili kukabiliana na kunguru ambao wamekuwa wakihangaisha wakazi na watalii.

Ndege hao weusi wenye kelele wamekuwa kero kwa miaka mingi kwa kuwa wanaweza kuwapokonya watu vyakula midomoni na hata kuwanyea vichwani wanapobarizi chini ya miti.

Kunguru ni ndege wanaopatikana katika miji mingi ya Pwani, ukiwemo mji wa Mombasa na hupenda kuishi sehemu zenye majaa ya takataka au kunakopatikana vyakula.

Hata hivyo, wamekuwa wakisumbua wakazi, kwa kuwa wakati mwingine huingia hata kwenye mikahawa na kuwapokonya watu vyakula.

Kwenye mswada wa kwanza wa bajeti ya mwaka 2018/19 ya kaunti, serikali ya Kaunti ya Mombasa sasa inapanga kutumia mamilioni kuwakomesha ndege hao.

Kuangamiza kunguru ni mojawapo ya hatua za serikali hiyo kwenye Wizara ya Mazingira, japo haijafafanuliwa mbinu zitakazotumiwa.

Lakini wahudumu katika sekta za utalii na safari za ndege wamepongeza pendekezo hilo. Maneja wa Uwanja wa Ndege wa Moi mjini Mombasa, Bw Walter Agong, alisema kuhamishwa kwa jaa la taka la Kibarani hadi Mwakirunge ni tishio kwa sekta ya usafiri wa ndege.

Hii ni kwa sababu kunguru hupaa juu na kuingia kwenye njia ya ndege.

Mwenyekiti wa muungano wa wahudumu wa hoteli Sam Ikwaye alisema kunguru ni kero kubwa sana kwa sekta ya utalii.

Hata hivyo aliitaka serikali ya Kaunti kushirikiana na wawekezaji kama shirika la Wanyamapori nchini (KWS) na lile la mazingira (Nema) ili kufanikisha mradi huo wa kuangamiza ndege hao. Walisema kunguru huhamia sehemu ambapo kuna vyakula na wakati sehemu moja haina chakula wanarudi Mombasa.

“Wanakosesha watalii starehe katika pwani ya Kenya, wajua sisi kama wawekezaji huw atunauza bidhaa nyingi sana zautalii ikiwemo mazingira. Lkaini watalii ambao huja humu nchini kuangalia ndege wanashindwa sababu kunguru wamekula vindege vyengine na mayai yao,” akasema Bw Ikwaye.

Alisema kunguru hao pia wanawakosesha watalii starehe hususan wanapobarizi wakiwadonadona.

“Ni vigumu kufanya sherehe za nje Mombasa sababu ya kurabu. Tumbili pia wanasumbua katika sekta ya usafiri wa ndege. Kurabu wanawapa changamoto kubwa sana wawekezaji wa sekta ya usafiri wa ndege,” akasema Bw Ikwaye.

Serikali ya kaunti ya Mombasa ilisema itachukua muda wa  miaka mitano kuangamiza ndege hao kwanzia mwaka huu hadi 2022. Mradi huo utatekelezwa katika mitaa yote ya kaunti hiyo ya kitalii ya Mombasa.

 

Habari zinazohusiana na hii

Joho awindwa na EACC