Siasa

David Ndii: Si dhambi kushirikiana na Ruto kutwaa urais 2022

October 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA FAUSTINE NGILA

MWANAUCHUMI maarufu Dkt David Ndii ametangaza kuwa huenda akashirikiana na Naibu Rais Dkt William Ruto kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Akihojiwa na gazeti la Saturday Nation Jumamosi, Dkt Ndii alisema ako tayari kwa ushirikiano huo iwapo utasaidia kuzima mpango wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Bw Raila Odinga wa kubatilisha katiba ili kufaidi watu wachache.

Alimlaumu Rais kwa kumsukuma Dkt Ruto kuanza kampeni za 2022 mapema, majuzi akiwapa vijana rukwama za bure, akisema Rais amekuwa akimtenga kwenye sera zake na hivyo kuwafanya wananchi kukubali falsafa yake ya ‘uhasla’.

“Wanaosema kuwa ninamuunga mkono Dkt Ruto wanajaribu kubadili mjadala muhimu. Siasa za Ruto zinakubalika na mamilioni ya Wakenya masikini, na anazifanya kwa wakati unaofaa. Rais ndiye amesababisha haya yote,” akasema.

Msomi huyo alisema kuwa wazo la Mpango wa Maridhiano (BBI) haufai kabisa kwa kuwa unalenga kuyaleta pamoja makabila matano makuu nchini ambao ni asilimia 75 ya nchi ili kuyatawala makabila 37.

“Tunataka kuwakomesha kutekeleza mpango huu. Tunalenga kuhakikisha uchaguzi utakuwa huru na wa haki kupitia katiba ya sasa. Nina uzoefu wa kujua ni nani nitashirikiana naye. Ukitzama takwimu za sasa, Dkt Ruto ndiye anayeweza kuibuka rais. Ana ufusasi wa asilimia 40 ya Wakenya, asilimia 25 hawana msimamo ilihali asilimia 35 wanaunga mkono Bw Odinga. Iwapo tutapata asilimia 65 ya kura zote, basi tutashinda uchaguzi,” akasema kwenye mahojiano hayo.

Kuhusu kusutwa mitandaoni kwa ushirikiano wake na Dt Ruto, Dkt Ndii aliwakumbusha wakosoaji kuwa chama cha Narc na muungano wa Nasa vilikuwa na wanasiasa wasiofaa.

Alipoulizwa kuhusu mwendendo wa Ruto kuonekana ‘akiwahonga’ wapigakura miaka miwili kabla ya uchaguzi, msomi huyo alisema kila mwanasiasa ana mbinu yake ya kuteka mioyo ya wananchi.

“Hiyo ndiyo mbinu yake, kuwasaidia masikini. Lakini pia nimejionea wanasiasa wakitoka makao makuu ya ODM na Ikulu wakiwa na hela nyingi mfukoni. Je, ni vizuri tu wakati mabwanyenye wanapewa mamilioni ya bure na ni dhambi kwa masikini kupewa rukwama? Na baadhi ya pesa huende ni zile zinaibwa katika hazina ya kupambana na corona. Huu ndio ubinafsi ambao nataka ukome,” alieleza.