• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
NGILA: Facebook ikague habari zake zisipotoshe mabilioni

NGILA: Facebook ikague habari zake zisipotoshe mabilioni

NA FAUSTINE NGILA

UFICHUZI wa hivi majuzi wa shirika la uanaharakati la Avaaz, Amerika kuwa Facebook iliachilia habari feki kuchapishwa katika mtandao wake na kufikia mabilioni ya watu, umeanika maovu yanayofanyika mitandaoni.

Takriban watu bilioni 3.8 waliwekwa kwenye hatari ya kupokea habari za kupotosha kuhusu mbinu za kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali, Covid-19 ikiwemo, katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.

Ingawa teknolojia ina manufaa yake mengi, inapotumiwa kutoa habari zinazopelekewa watu kufanya maamuzi yanayotishia maisha yao, basi teknolojia hugeuka kuwa silaha ila wa kulaumiwa ni wanaoitumia kwa malengo hayo.

Iweje tovuti kumi zilikubaliwa kusambaza habari feki na Facebook na habari hizo kutazamwa mara nne zaidi kuliko habari katika kurasa za Shirika la Afya Duniani (WHO) linalotoa habari za kuaminika?

Ni aibu kwa Facebook kuruhusu taarifa iliyodai kuwa Bill Gates aliunga mkono chanjo ya polio iliyosababisha watoto 500,000 nchini India kupooza, kusalia katika seva zake na kutazamwa mara milioni 8.4. Pia taarifa feki iliyodai kuwa vituo vya karantini vilikuwa tisho kwa afya ya umma ilitazamwa mara milioni 2.4.

Kampuni hii, ambayo katika miezi sita iliyopita iliandaa warsha za mitandaoni kuarifu watu dhidi ya habari feki, inafaa kuonyesha mfano bora, kwa kung’oa habari zote feki katika mtandao wake.

Kwa kuwa imewekeza vilivyo katika teknolojia ya data, Inafaa kuwa na idara nzima ya kufuatilia ukweli katika kila habari inayochapishwa na kila mtumizi wa mtandao huo.

Licha ya kujitetea kuwa iliweka ilani za kuonya watu dhidi ya taarifa feki kuhusu corona kwa viungo milioni 98 mtandaoni, baadhi wa watu duniani wamepoteza maisha yao baada ya kubugia sabuni ya kuosha vyombo iliyochanganywa na pombe, kutokana na taarifa walizosoma kwenye mtandao huo.

Kenya, ambayo tayari ina watumizi wa Facebook zaidi ya milioni 7, haisazwi katika vita dhidi ya taarifa za kupotosha. Kutokana na machapisho ya watu katika Facebook, kumekuwa na imani potovu kuwa virusi vya corona havipo, na ni njama ya serikali ya kuomba misaada ya kifedha.

Facebook, inafaa kuchapisha maelezo ya kufafanua kuhusu ugonjwa huo kwa maelfu ya watu wanaoamini upuuzi huo, ili kuondoa uwezekano wa watu kufariki kwa kukosa kuelewa.

Pia, ni jukumu la kampuni hiyo, ambayo pia ni chombo kikuu cha habari, kuwatumia watumizi wake ilani kuwaonya dhidi ya nadharia potovu zinazoenezwa mitaani na kuchangia watu kufanya maamuzi hatari.

Kupitia uchanganuzi wa data, hii ni kampuni yenye uwezo wa kuzika kila aina ya habari feki katika mtandao wake na kufanya duniani kuwa pahali salama pa kuishi.

Bw Ngila ni mhariri wa habari katika tovuti ya Taifa Leo

[email protected]

You can share this post!

AWINO: Wakulima hawana cha kujifutia jasho, wanapunjwa tu

WANDERI: Mikopo hii ya kigeni imegeuka utumwa