MUTUA: Itakuwa kibarua kudhibiti Trump na Biden mijadalani
Na DOUGLAS MUTUA
NIMETAFAKARI kuhusu mojawapo ya mbinu ambazo zinapendekezwa ili kumdhibiti Rais Donald Trump wa Marekani wakati wa midahalo ya urais nikajipata nikiangua kicheko na kusema ‘kila la heri’!
Tume inayoandaa midahalo ya urais nchini Marekani imependekeza kuzima kipaza sauti cha ama Bw Trump au mpinzani wake, Bw Joe Biden, mara tu mmoja wao anapopewa fursa ya kuzungumza.
Haja ya kuzima kipaza sauti kimoja imeibuka ghafla baada ya mdahalo wa wiki jana kutokea kuwa kituko kitupu kutokana na kelele za Bw Trump.
Kila mshiriki alipewa dakika mbili pekee za kuzungumza kwa zamu na mfawidhi Chris Wallace, lakini Trump alifoka kiholela na kumtatiza Bw Biden, ambaye wakati mmoja alipandwa na wa kwao na kumwambia Rais wa watu: “Fyata mdomo bwana!”
Juhudi za Bw Wallace kuingilia kati kama msimamizi wa mdahalo wenyewe hazikufaa kifu; Trump alikwenda sambamba naye, mwishowe akaishia kuizamisha sauti ya mfawidhi huyo.
Watu wengi waliotazama mdahalo huo walisema haukuafiki kuitwa mdahalo wa urais bali kelele za kitoto kwa sababu haukuwa na ustaarabu wowote.
Baadhi yao walilalamika kuwangwa na vichwa, wengine kuumwa na masikio, sikwambii hata wapo walioshangaa walipoteza usingizi wao kwa dakika 90 wakitizama kitu gani.
Wote waliokasirishwa na yaliyotokea usiku huo walimlaumu Trump, mtu asiye na subira hata ya sekunde mbili, kwa kuigeuza shughuli hiyo muhimu kuwa kioja cha kuudhi. Nilisema ‘kila la heri’ pale tume inayosimamia midahalo ya urais ilipotishia kuzima kipaaza sauti kimoja kwa sababu namjua Trump: haambiliki hasemezeki!
Hata kipaza sauti chake kikizimwa, atafoka kama kichaa sokoni na kumtatiza mwenzake atakayekuwa umbali wa mita mbili pekee.
Bila shaka vipaza sauti vya enzi hii ya dijitali vina wigo mkubwa hivi kwamba hata ukiangusha sindani vinanasa sauti ya mwanguko huo na kuuvumisha mbali.
Ikiwa sauti ya sindano inasikiza, seuze kelele za Trump ambazo kawaida hufanywa makusudi kuwatishia na kuwadhalilisha watu asiokubaliana nao? Hapo pana kibarua kigumu tu.
Trump si mwanasiasa wa kawaida anayehofia kujiharibia sifa; dakika mbili ni nyingi mno kwake, hivyo anaweza kuamua kujongea kipaza sauti cha mwenzake na kutema tusi au kuvuruga mambo ilmuradi tu utawala wake mbaya wa miaka minne iliyopita usikosolewe.
Kumbuka wakati wa mojawapo wa midahalo aliyoshiriki na Bi Hillary Clinton mnamo 2016, Trump alimfuata nyuma Bi Clinton kwa njia ya kutishia pindi Bi Clinton alipokuwa akihutubia watu waliohudhuria hafla hiyo.
Bi Clinton alisema baadaye kwamba aliingiwa na woga sana alipogundua Trump alikuwa nyuma yake kwa sababu chochote kingeweza kutokea.
Trump na jeuri yake ni mtu asiyetabirika kwa hakika. Unachoweza kutabiri kumhusu ni kwamba wakati wote atafanya mambo visivyo.
Jambo linalozuga akili za kila mtu mstaarabu ni kwamba Trump na ukorofi wake huo anavutia mamilioni ya watu! Wafuasi wake, na hata baadhi ya washauri ambao ni wahafidhina kindakindaki, wanampenda alivyo, tena wangetaka aendelee kuvuruga mambo.
Je, akijongea kipaza sauti, au afoke kwa mbali na kutatiza mjadala utakaofanyika wiki mbili zijazo, waandalizi watamfanyia nini? Hamna!
Bila shaka hawawezi kumwitia polisi wamdhibiti kwa maana hiyo itakuwa aibu ya kimataifa. Njia ambayo kwayo Trump anaweza kudhibitiwa vizuri ni kumweka yeye na Biden kwenye vyumba viwili tofauti ila vyenye mafundi wa mitambo wa tume husika ili kila mmoja asipate fursa ya kukaribia kipaza sauti cha mwenzake hata kidogo.
Wote wawili wanaweza kuwekuwa viwambo kama vya runinga mbele yao ili waonane na kuhisi kana kwamba wanazungumziana.
Njia nyingine ila hatari ni ya kuwaweka kwenye chumba kimoja, kipaza sauti cha asiyezungumza kizimwe, Trump akijongea cha mwenzake tu mdahalo umalizwe ghafla kwa maelezo kwamba Rais hadhibitiki. Hapo atapata fedheha na lawama kwa mkumbo mmoja, hali atakayojutia mno kwa kumnyima ushindi kura zikipigwa Novemba 3.