Habari Mseto

Wakazi wa Marakwet waomboleza Padre Reinhard Bottner aliyewaletea 'mwanga' wa elimu, imani ya dini na huduma za afya

October 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na EVANS KIPKURA

PADRE raia wa Ujerumani, Reinhard Bottner alipotumwa Kenya kwa shughuli za kimisheni mnamo 1975, alijipata katika eneo la Embotut, Marakwet Mashariki.

Eneo hilo lilikuwa halipitiki kirahisi na visa vya upashaji tohara kwa wasichana vilikuwa vya kiwango cha juu.

Hizi ni miongoni mwa changamoto ambazo Bottner, 46, alilazimika kupitia katika kibarua chake cha kwanza cha kimataifa nje ya bara Ulaya.

Kwa kipindi cha miongo mitano, Bottner alikusanya rasilmali muhimu kutoka kwa viongozi na mashirika mbalimbali ya kidini ili kutoa majukwaa muhimu kwa masuala ya elimu, kilimo, ufugaji na ujenzi wa miundo-msingi muhimu.

Kasisi Bottner aliaga dunia katika Hospitali ya Mater Misercordiae, Nairobi mnamo Septemba 29, 2020 akiwa na umri wa miaka 86. Hadi kifo chake, alikuwa amelezwa katika hospitali hiyo kwa kipindi cha wiki mbili.

Kwa mujibu wa taarifa Kasisi Mkuu William Kipkemboi Kosgey wa Dayosisi ya Kanisa Katoliki la Eldoret, mipango ya mazishi ya Bottner inaendelea kwa sasa.

“Tunatoa rambirambi zetu na kuombea familia nzima ya wamisheni wa Benedictine. Tunaomba Mola aifariji familia ya Bottner katika kipindi hiki kigumu,” ikasema sehemu ya taarifa hiyo.

Licha ya kujihusisha na masuala mengi ya kimisheni, ambacho Kasisi Bottner anakumbukwa kwayo katika eneo la Marakwet Mashariki na Keiyo Kusini ni ukubwa wa mchango wake katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Mengi ya makanisa ambayo yamejengwa na Kasisi Bottner katka maeneo hayo kwa sasa ni vivutio vya utalii huku Kanisa la St Kizito Wewo Embobut likisifiwa sana kwa upekee wa mtindo wa kisanaa uliotumiwa katika ujenzi wake. Kanisa hilo limejengwa kwa umbo la njiwa.

Bottner alitumia pia mtindo wa usanifu majengo uliotamalaki ujenzi wa makanisa nchini Ujerumani katika miaka ya 1970 kujenga makanisa Katoliki ya Lemeiywo, Korou, Kapchebau, St Michael na Kamwosor.

Mchango wa Bottner pia ulikuwa mkubwa katika ujenzi wa Hospitali ya St Michael na Shule ya Msingi na ya Upili ya St Michael Embobut.

Julius Belator, ambaye alikuwa msaidizi na mpishi wa Kasisi Bottner kwa kipindi cha miaka 40 alisema amepoteza mtu ambaye alikuwa sehemu ya maisha yake duniani.

IMETAFSIRIWA NA: CHRIS ADUNGO