Sabina Chege lawamani kuhusu ghasia na kifo Murang'a
Na CHARLES WASONGA
MBUNGE wa Kiharu Ndindi Nyoro amedai kuwa wanasiasa kadha kutoka Murang’a wakiongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti hiyo Sabina Chege ndio walipanga vurugu zilizoshuhudiwa katika Kanisa la AIPCA eneo la Kenol ambapo mtu mmoja aliuawa.
Naibu Rais Dkt William Ruto alihudhuria ibada ya Jumapili na mchango wa fedha katika kanisa hilo.
Akiongea Jumapili mjini Kenol baada ibada hiyo Bw Nyoro alidai kuwa Bi Chege ndiye aliwakodi wahuni walioziba barabara na kusababisha fujo kabla ya Dkt Ruto kuwasilisha katika Kanisa hilo.
“Ningependa kuwaambia kuwa ni Mama wa Kaunti hii ambaye aliwalipa vijana waliobabisha vurugu siku ya leo ambapo Naibu Rais alitutembelea. Najua pamoja na wakora wengine walikutana katika hoteli moja Thika kupanga vurugu hizi,” akasema.
Akaongeza: “Ningependa kuwaambia kwamba wakome kuwatumia watoto wa wengine kuzua fujo. Waleta watoto wao na wake zao waandamane,”
Naye Mbunge wa Kandara Esther Wahome ambaye alikuwa mwenyeji wa Dkt Ruto, alisema kuwa alimpigia simu Kamishna wa Kaunti kumjulisha kuhusu mipango ya watu fulani kuchochea maandamano ili kuvuruga ziara ya Naibu Rais, lakini hakuchukua hatua zozote.
“Nilimpigia simu mara tatu lakini hakushika. Ningetaka kumwambia kwamba nilikuwa na habari kwamba kuna watu waliopanga maandamano. Lakini tungetaka kuwaambia kwamba nguvu za shetani zimeshindwa,” akaeleza Bi Wahome.
Jumapili asubuhi, shughuli zilisitishwa katika barabara ya Kenol- Murang’a fujo zilipotanda na kupelekea watu wengi kujeruhiwa.
Hata hivyo, utulivu ulirejea mwendo wa saa nne za asubuhi na ibada ikaendelea japo taharuki ilitanda nje na ndani ya kanisa hilo.
Akiongea baadaye mjini Kenol Dkt Ruto aliwalaani waliochochea fujo hizo akisema vitendo kama hivyo havitaathiri azma yake ya kuingia Ikulu.