• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
MKU, Posta zaingia katika maelewano ya ushirikiano

MKU, Posta zaingia katika maelewano ya ushirikiano

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kimeingia katika mkataba wa ushirikiano na Posta pamoja na TV 47.

Shirika la Posta Corporation of Kenya, MKU na TV47 zilitia saini mkataba wa maelewano ya ushirikiano mnamo Ijumaa wiki jana ili kujiendeleza zaidi kimaendeleo.

MKU itajiendeleza zaidi kwa kutoa mafunzo kwa wanafunzi hasa katika utafiti na kufikia wananchi mashinani.

Nayo TV 47 kupitia mawasiliano itakuwa na umuhimu wa kuangazia matukio tofauti yanayotendeka sehemu tofauti.

Mkurugenzi wa shirika la Posta Bw Daniel Kagwe, alisema kuwa shirika lake litakuwa mstari wa mbele kuwaajiri wanafunzi watakapokamilisha masomo yao katika viwango tofauti kutoka MKU.

“Tutafanya ushirikiano wa karibu na wanafunzi hao kwa kuwapa nafasi ya kutafuta soko la vifaa vyetu na kuendesha majaribio ya masomo yao katika shirika letu,” alisema Bw Kagwe.

Alisema maswala muhimu watakaojihusisha nayo ni M-posts, EMSSGO na E-Njiwa.

Alisema katika kipindi kilichoko, mashirika mengi yanazingatia ushirikiano wa pamoja na sekta nyinginezo ili kujiendeleza kwa njia iliyo bora.

“Tutahakikisha tunafanya kazi na wanafunzi wa MKU ili waje na ubunifu mpya utakaotuweka katika soko la kiuchumi. Nacho kituo cha kupeperusha habari cha TV 47 kitakuwa mstari wa mbele kutuangazia matukio tofauti yanayotendeka humu nchini na maeneo mengine,” alisema Bw Kagwe.

Alisema shirika hilo litakuwa na uwezo kamili wa kusambaza shughuli zake katika serikali kuu na sekta ya wamiliki binafsi.

Bw Kagwe alisema watajiunga pamoja na wanafunzi wanaojishughulisha na michezo ili kutafuta vipaji kutoka kwao na kuwaajiri hapo baadaye.

Kudumu

Mkurugenzi mkuu wa wa shirika la runinga la TV47, Bw Abdulahi Abubakar alisema ushirikiano huo ni wa kudumu na atahakikisha wanatoa huduma ya kuridhisha katika Posta na MKU.

“Shirika letu tayari limesambaa katika kaunti zote 47 na lengo letu kuu huwa ni kupeperusha habari sahihi na pia kuelimisha wananchi kwa maswala mengi tofauti. Pia tunalenga sana kushirikiana na vijana mashinani,” alisema Bw Abubakar.

Naibu chansela wa MKU Prof Stanley Waudo  alisema chuo hicho kimekuwa mstari wa mbele kufikia wananchi walioko mashinani huku wakitoa misaada.

“Chuo chetu pia kinaweka mkazo kwa wanafunzi kikiwahimiza wawe wabunifu ili waweze kujitegemea vilivyo wanapokamilisha masomo yao ya chuoni,” alisema Prof Waudo.

Alisema chuo hicho pia kimekuwa na ushirikiano na hospitali ya Thika Level 5. Hata walijenga chumba cha kuhifadhi maiti cha General Kago Funeral Home, ambako wanafunzi pia wanaendesha mafunzo yao ya udaktari.

Wameweza pia kushirikiana na mashirika mengine ya kigeni.

You can share this post!

Migori yachagua Spika mpya

Spurs wadhalilisha Man-United kwa kichapo cha 6-1 katika...