Habari Mseto

Afisa wa Harambee Sacco akana kuiba mamilioni

May 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Afisa wa chama cha akiba na mikopo cha Harambee, Walter Bonyo akiwa kizimbani Jumatatu. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA mkuu katika chama cha akiba na mikopo chenye wanachama wengi zaidi nchini cha Harambee Sacco alishtakiwa Jumatatu kwa wizi was Sh12.3 milioni.

Bw Walter Obunga Bonyo alikanusha aliiba pesa hizi kutoka kwa chama hiki ambacho wanachama wake ni watumishi wa umma kutoka idara za kijeshi, polisi , magereza na wizara za serikali.

Bw Bonyo alikanusha shtaka kwamba kati ya  Desemba 1 2017 na Feburuari 7 2018 akishirikiana na wengine aliiba Sh12,350,000 mali ya Hatrambee Sacco.

Kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha alimweleza hakimu mkuu Bw Francis Andayi kuwa kesi dhidi ya Bw Bonyo itaunganishwa na kesi nyingine tatu zilizoorodheshwa kusikizwa mnamo Agosti 6, 2018.

Bw Naulikha alimweleza hakimu kuwa washukiwa wengine walioshtakiwa kuhusiana na wizi huo awali waliachiliwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh300,000.

Mahakama ilielezwa kesi dhidi ya washukiwa hao wengine itatajzwa mnamo Julai 3 ndipo kesi zote ziunganishwe.

Bw Andayi aliagiza kesi dhidi ya Bw Bonyo itajwe siku hiyo ya Julai 3, 2018 iunganishwe na hizo nyingine.

Pia aliagiza mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana sawa na hiyo iliyopewa washukiwa walioshtakiwa hapo awali.

Kiongozi wa mashtaka alisema nakala za mashahidi ziko tayari na ikiwa mshukiwa yuko tayari anaweza kupewa nakala pamoja na mashtaka dhidi ya washukiwa wale wengine.