• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
Mhalifu avamia kasri la Ronaldo na kuiba jezi na bidhaa za thamani isiyojulikana

Mhalifu avamia kasri la Ronaldo na kuiba jezi na bidhaa za thamani isiyojulikana

Na MASHIRIKA

KASRI linalomilikiwa na mwanasoka Cristiano Ronaldo mjini Madeira, Ureno lilivamiwa na mhalifu aliyeiba bidhaa za thamani isiyojulikana usiku wa Oktoba 7, 2020.

Ronaldo, 35, alikuwa amesafiri nchini Uhispania kuongoza timu ya taifa Ureno kucheza mechi ya kirafiki na Uhispania wakati wa tukio hilo.

Mchumba wa Ronaldo, Georgina Rodriguez, hakuwa pia katika kasri hilo la thamani ya Sh980 milioni kwa sababu alikuwa akishiriki hafla ya uanamitindo na fasheni jijini Paris, Ufaransa.

Kwa mujibu wa gazeti la Diario de Noticias Madeira, watoto wa Ronaldo walikuwa wameachwa chini ya uangalizi wa mama yake, Dolores Aveiro.

Dolores, 65, anaishi na wanawe wengine watatu – Elma, Katia na Hugo katika mtaa wa kifahari wa Funchal, mbali kidogo na eneo la Madeira.

Kwa mujibu wa maafisa wa polisi mjini Madeira waliomhoji jamaa mmoja wa Ronaldo, mhalifu huyo ambaye ni mtu anayejulikana kwake, alipata fursa ya kuingia kwenye kasri la Ronaldo kupitia eneo la gereji.

Madai hayo yalithibitishwa na maafisa wa polisi ambao wameanza msako baada ya kurejelea video iliyonaswa na kamera za CCTV.

Kati ya bidhaa Ronaldo aliibiwa ni jezi za kikosi cha Juventus kinachoshiriki soka ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Gerard Pique wa Barcelona na fowadi wa zamani wa Chelsea, Alvaro Morata ni miongoni mwa wanasoka ambao makasri yao yamevamiwa na majambazi hivi karibuni wakati wakiwajibika uwanjani.

You can share this post!

Matiang’i apewa mamlaka zaidi ya kudhibiti mikutano...

Montreal Impact yazoa ushindi wa kwanza katika mechi 6,...