• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:04 PM
Utawala wa mpito waachilia huru wanajeshi, wanasiasa

Utawala wa mpito waachilia huru wanajeshi, wanasiasa

Na AFP

BAMAKO, Mali

WANASIASA na wakuu wa kijeshi waliokamatwa wakati wa mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini Mali mnamo Agosti 18, jana waliachiliwa huru na utawala wa mpito.

Kati ya walioachiliwa ni aliyekuwa Waziri Mkuu, Boubou Cise ambaye alihudumu kwenye serikali ya Rais aliyeondolewa madarakani, Ibrahim Boubacar Keïta.

Mkuu mpya wa kijeshi Assimi Goita alitoa taarifa Jumatano akisema, viongozi wa kisiasa walionyakwa wakati wa mapinduzi hayo wameachiliwa huru. Hata hivyo mienendo yao itakuwa ikifuatiliwa kwa karibu ili wawajibike panapotokea haja ya kuwafikisha kortini.

“Wameachiliwa huru lakini watasalia kwenye darubini yetu ili wanapohitajika kortini kujibu mashtaka basi wanafikishwa na kujibu mashtaka hayo,” akasema Goita.

Aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa la Mali, Moussa Timbine alikuwa miongoni mwa majenerali wanane ambao waliachiliwa huru na serikali hiyo ya mpito.

Waasi waliopindua serikali ya Mali ndio wanaongoza serikali ya mpito huku taifa hilo likitarajia uchaguzi uandaliwe baada ya miezi 18. Inakisiwa hatua ya kuwaachilia wanajeshi waliohudumu kwenye utawala wa Rais Keita ni sehemu ya kukuza juhudi za upatanishi na kuleta amani.

Mnamo Jumatatu, serikali ya mpito ya kurejesha utawala kwa raia ilibuniwa huku Goita akichaguliwa vilevile kama Makamu wa Rais kutokana na juhudi zake kwenye mapinduzi yaliyong’oa utawala wa Rais Keita.

Vilevile, Muungano wa Kiuchumi wa Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) uliondoa vikwazo vya kibiashara dhidi ya Mali ukisema, nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha kwamba utiluvu upo na mkondo wa marekebisho ya katiba unaendelea kuafikiwa.

Muungano huo pia ulisifu uteuzi wa kanali mstaafu Bah Ndaw kama Kaimu Rais na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni, Moctar Ouane kama Waziri Mkuu mpya wa serikali ya mpito inayotarajiwa kudumu kwa miezi 18 kabla ya mamlaka kukabidhiwa raia.

Rais Ndaw tayari amewateua mawaziri 25 kuiongoza serikali ya mpito ambayo jukumu lake kuu litakuwa kuhakikisha uchaguzi mpya unafanyika baada ya muda uliokubaliwa.

Hata hivyo, wizara muhimu za Ulinzi, Usalama, Utawala wa Kieneo na ile ya Upatanishi wa Kitaifa zilitwaliwa na maafisa wa jeshi huku raia wakiteuliwa kwenye nyadhifa za wizara ya Katiba na ile ya Masuala ya Kigeni.

You can share this post!

Isuzu East Africa kumpokea Kipchoge kishujaa wiki ijayo

DOMO KAYA: ‘Kakinuka, acha kanuke’