• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
IG atetea polisi wavunjao mikutano ya kisiasa

IG atetea polisi wavunjao mikutano ya kisiasa

Na BENSON MATHEKA

INSPEKTA Jenerali wa polisi, Hillary Mutyambai, ametetea hatua ya polisi ya kumnyima Naibu Rais William Ruto kibali cha kuandaa mikutano ya kisiasa huku wakiwaruhusu viongozi wengine kufanya hivyo.

Polisi wamekuwa wakinyima washirika wa Dkt Ruto vibali vya kuandaa mikutano ya hadhara, ikiwemo ya harambee makanisani huku wakiruhusu wanasiasa wengine kuandaa mikutano inayohudhuriwa na maelfu ya watu.

Bw Mutyambai alisema polisi huwa wanaruhusu mikutano kufanyika baada ya kuhakikisha kuwa hakuna hatari ya ghasia kuzuka au kundi moja kushambuliwa.

“Nimeona malalamishi kuhusu ubaguzi katika utekelezaji wa sheria kuhusu mikutano ya umma. Polisi huwa wanaruhusu mikutano ya umma baada ya kuhakikisha hakuna hatari ya ghasia au shambulizi kwa kundi fulani,” alisema Bw Mutyambai.

Akijibu maswali kutoka kwa umma kupitia Twitter jana, Bw Mutyambai alisema polisi huwa wanakataa kuruhusu mikutano wakitambua kuna hatari ili kulinda umma na mali.

“Kuna makundi ambayo hayajahusika na aina yoyote ya ghasia huku mengine yakihusishwa na fujo na hii ndio sababu kumekuwa na tofauti katika utoaji wa vibali,” alisema Bw Mutyambai.

Dkt Ruto na washirika wake walilaumu polisi kwa ubaguzi wakisema, kanuni zilizotangazwa na kamati ya kitaifa ya ushauri wa usalama (NSAC ) wiki jana zililenga kumzima.

Kulinganana na kanuni hizo, waandalizi wa mikutano ya kisiasa wanafaa kuomba kibali kutoka kwa maafisa wanaosimamia vituo vya polisi eneo wanalopanga kufanyia mkutano siku tatu kabla ya tarehe ya mkutano.

Licha ya wandani wa Dkt Ruto kufanya hivyo huko Kakamega, polisi walifuta mikutano miwili mwishoni mwa wiki.

Kauli ya Bw Mutyambai ilikosolewa vikali na wanasheria ambao wanasema kanuni za NSAC ni ukiukaji wa haki ya kukusanyika. Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK), Nelson Havi, alisema polisi hawana nguvu za kikatiba kuzuia mikutano.

“Katiba inaruhusu uhuru wa kukutana lakini sasa wanatuambia mikutano ni haramu. Hawana mamlaka ya kufuta mikutano,” alisema Bw Havi. Kuanzia Alhamisi wiki jana, polisi walifuta mikutano sita ya Dkt Ruto na washirika wake kaunti za Kisii, Nyamira, Kwale na Kakamega.

Waliruhusu kiongozi wa ODM Raila Odinga kufanya mikutano kaunti ya Kisii, Migori na Siaya. Ingawa walisingizia kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona na hatari kwa usalama, mikutano ya Bw Odinga ilihudhuriwa na maelfu ya watu ukiwemo aliotembelewa na ujumbe wa wazee zaidi ya 700 kutoka jamii ya Agikuyu nyumbani kwake Bondo.

Viongozi wengine, akiwemo mwenyekiti wa chama cha Kanu Gidion Moi na mgombeaji wa ODM katika uchaguzi mdogo wa Msambweni, waliruhusiwa kufanya mikutano huku washirika wa Dkt Ruto wakinyimwa vibali na kurushiwa gesi ya kutoa machozi.

Wataalamu wa masuala ya utawala wanasema kutumiwa kwa polisi kuzima mikutano ya baadhi ya wanasiasa na kuruhusu ya wengine ni hatari.

“Tumeona polisi wakitumiwa kusimamisha mikutano kwa misingi ya kisiasa na sio kisheria. Hii sio hatua nzuri kwa nchi inayoelekea kwa uchaguzi,” asema mtaalamu wa utawala David Owino.

Anasema polisi wanafaa kudumisha usalama katika mikutano ya kisiasa baada ya kufahamishwa walivyofanya Bw Odinga alipokuwa Kisii na Bondo.

You can share this post!

Ngilu kusambaza barakoa bila malipo kwa wanafunzi 72,000

Madereva wa malori wakashifu Macharia