• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 9:12 AM
Wafuasi wa Ruto wasema hawatatishika

Wafuasi wa Ruto wasema hawatatishika

Na VITALIS KIMUTAI

WANDANI wa Naibu Rais, Dkt William Ruto, wameapa kuendelea na kampeni za katika maeneo mbalimbali nchini, licha ya masharti makali yaliyowekwa na serikali dhidi ya mikutano ya hadhara.

Kauli hiyo imejiri huku msako mkali ukiendelea dhidi ya mikutano miwili katika maeneo ya Nyanza Kusini na Pwani ambayo Dkt Ruto alitarajiwa kuhudhuria.

Mbunge wa Sotik Bw Dominic Koskei na mwenzake wa Bureti Bw Japeth Mutai walisema hawatatiwa woga kusitisha mikutano yao na makundi ya kidini, vijana, wanawake na wasiojiweza na makundi ya kidini, wanawake na wasiobahatika.

“Tutatimiza masharti ambayo yamewekwa na serikali na tutaendelea na mikutano yetu kote nchini. Ni haki ya watu kikatibu kukusanyika,” alisema Bw Koskei.

Alisema hatua ya kulemaza umaarufu wa Bw Ruto kote nchini haitafaulu kwa sababu watu mashinani wanamuunga mkono.

“Baada ya kutawanya mkutano Nyamira, nataka kuwaeleza mahasidi wa Dkt Ruto kwamba safari hii watu watatembea kutoka Nyanza Kusini hadi katika eneo la mkutano Kusini mwa Bonde la Ufa na hakuna vitisho vitakavyozuia hatua hii,” alisema.

Wafuasi wa Naibu Rais walimtetea kuhusu kutoa zawadi ikiwemo kuku, toroli na mashine za kushonea nguo kwa vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini, akisema ni mradi wa uimarishaji unaopaswa kuungwa mkono na watu wote.

Mbunge wa Bahati, Bw Kimani Ngunjiri alitoa wito kwa Wakenya kutetea vikali haki yao ya kukusanyika na uhuru wa kujieleza unaoruhusiwa katika Katiba.

“Inasikitisha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita vigogo wa kisiasa na baadhi ya maafisa wakuu wa umma wamepania kuhujumu hatua za kidemokrasia zilizofanikishwa katika katiba mpya inayotazamiwa kufanyiwa marekebisho,” alisema Bw Ngunjiri.

Dkt Ruto anakabiliwa na kibarua cha kuchukua usukani wa chama cha Jubilee kabla ya uchaguzi wa 2022.

Bw Mutai alidai kuwa washindani wa Naibu Rais wameingiza baridi kutokana na kuongezeka kwa umaarufu wake miongoni mwa watu mashinani.

“Tumekubaliana kuendelea kupambana na kuzidi kutilia maanani shabaha letu ambalo ni kunyakua urais 2022 licha ya vikwazo vyote vilivyowekwa njiani. Vizingiti vilivyowekwa vimeshajiisha watu kumuunga mkono Dkt Ruto,” alisema Bw Mutai.

Dkt Ruto anatarajiwa kuzuru kaunti za Kisii na Nyamira mwishoni mwa juma katika hafla zinazoandaliwa na Naibu Gavana wa Kaunti ya Kisii Joash Maangi na baadhi ya wabunge.

Mwakilishi Mwanamke katika Kaunti ya Kericho Florence Bore alisema ilisikitisha kwamba wasiri wake Rais Uhuru Kenyatta ndio wanaomhangaisha Naibu Rais licha ya mchango muhimu aliotoa kutwaa urais katika chaguzi kuu mbili zilizopita.

“Tunaishi katika nyakati za kushangaza mno kwa hakika wakati maafisa wa chama cha Jubilee wanamhangaisha hadharani hata bila haya Naibu Rais,” alisema Bi Bore.

Hivi majuzi, Dkt Ruto na wafuasi wake walifululiza katika makao makuu ya Chama cha Jubilee na kufanya mkutano katika kisa kilichozua dhoruba kisiasa nchini.

Bw Ruto amekuwa akitofautiana na Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju na naibu mwenyekiti wa chama hicho David Murathe kuhusu masuala kadhaa.

You can share this post!

Madereva wa malori wakashifu Macharia

Wazee wakemea matamshi ya chuki