Walimu wataka kila shule ipewe mhudumu wa afya
Na STEVE NJUGUNA
CHAMA cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo (Kuppet), kimeitaka serikali kupeleka wahudumu wa afya katika shule za msingi na sekondari ili kujiandaa kuwahudumia wanafunzi watakaopatikana na virusi vya corona.
Katibu wa Kuppet tawi la Laikipia, Robert Miano, alisema kuwa shule nyingi hazijatimiza matakwa yaliyowekwa na Wizara ya Elimu kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.
Bw Miano anataka kila shule kupewa mhudumu mmoja wa afya kwa ajili ya dharura zikitokea.
“Kila shule inafaa kuwa na mhudumu mmoja wa afya atakayewapima joto wanafunzi na kutoa huduma za dharura kunapotokea visa vya waathiriwa wa virusi vya corona,” akasema Bw Miano aliyekuwa akizungumza mjini Nyahururu.
Waziri wa Elimu, George Magoha ameagiza wakuu wa shule kuhakikisha kuwa wanaweka rekodi kuhusu wanafunzi walio na matatizo ya kiafya.
Lakini Bw Miano alisema kuwa walimu hawafai kutwikwa jukumu la kushughulikia afya ya wanafunzi.
“Walimu hawafai kupewa jukumu la kuangalia afya ya wanafunzi. Serikali ipeleke wahudumu wa afya shuleni ili kuwapa walimu fursa ya kufundisha,” akasema Bw Miano.
Wakat huo huo, Bw Miano alilalamika kuwa serikali haijatuma fedha katika shule za umma licha ya wanafunzi wa Gredi 4, Darasa la Nane na Kidato cha Nne kuanza masomo yao siku mbili zilizopita.
“Itakuwa vigumu kuweka mikakati ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona miongoni iwapo serikali haitatoa haraka fedha kwa shule za umma,” akasema.
Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kuwa nyingi ya shule zimeweka mikakati ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona miongoni mwa wanafunzi.