• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
Jumwa kujibu mashtaka ya mauaji

Jumwa kujibu mashtaka ya mauaji

Na RICHARD MUNGUTI

MBUNGE wa Malindi Aisha Jumwa sasa atafunguliwa mashtaka ya mauaji pamoja na mlinzi wake.

Afisa mkuu katika afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) eneo la Mombasa Bw Alloys Kemo , alitia sahini kibali cha kumfungulia mashtaka ya mauaji Bi Jumwa na mlinzi wake.

Kabla ya agizo la akamatwe na kushtakiwa kwa mauaji kutolewa ,Bi Jumwa  alikuwa amebashiri hayo punde tu alipokanusha mashtaka ya kula njama kufuja sehemu ya uwakilishi bungeni Malindi pesa za kulistawisha (NG-CDF) Sh19milioni.

Pia mbunge huyo anakabiliwa na shtaka la ubadhirifu wa pesa na kujinufaisha na pesa alizojua zilipatikana kwa njia isiyo halali.

Mwanasiasa huyo mbishi anadai masaibu yake yamechangiwa na msimamo wake wa kumuunga mkono naibu wa Rais Dr William Ruto katika azma yake ya kuwania urais mwaka wa 2022.

Mbunge huyo amesema mara si haba kwamba hakuna vitisho vitamfanya atupilie mbali msimamo wake wa kumuunga mkono Dkt Ruto katika safari yake ya kuelekea Ikulu.

Hivyo basi kuidhinishwa Bi Jumwa ashtakiwe kwa mauaji hakujamshtua kamwe, kwa vile alikuwa ametabiri mieizi miwili iliyopita kwamba “atafunguliwa shtaka hilo ambalo akipatikana na hatia aidha atasukumwa kifungo cha gerezani ama atahukumiwa kunyongwa.”

Akiwahutubia wafuasi wake nje ya Mahakama ya Mombasa aliposhtakiwa kwa ufisadi Bi Jumwa aliwaeleza kuwa “ amejiandaa kimawazo na moyoni kufunguliwa shtaka hilo.”

“Najua muda mwingi hautapita na wanaonipinga kisiasa watanishtaki kwa mauaji. Wanajaribu kunimaliza kisiasa lakini nawajulisha sitaogopa kamwe,” Ms Jumwa aliwafahamishwa wafuasi wake nje ya mahakama ya Mombasa alipokana mashtaka ya ufisadi mnamo Agosti 31.

Kwa mujibu wa afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma-ODPP-, mwanasiasa huyo atashtakiwa pamoja na Bw Geoffrey Okuto Otieno kwa mauaji ya Gumbao Jola.

Jola alikuwa mjombawe mwakilishi wa wadi ya Ganda (MCA) Bw Reuben Mwambize Katana.

Mfuasi huyo wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) aliuawa baada ya rabsha kuzuka usiku ambapo Bi Jumwa na wafuasi wake walipovamia zoezi lililokuwa limeandaliwa na wanachama wa ODM.

“Kinara wa masuala ya mashtaka eneo la Mombasa Bw Alloys Kemo alihidhinisha shtaka la mauaji dhidi ya Bi Aisha Jumwa na Bw Geoffrey Okuto Otieno kufuatia shambulizi dhidi ya Gumbao Jola mnamo Oktoba 2019 ambapo watu kadhaa walijeruhiwa,”ilisema taarifa ya mtanda0 wa Twitter wa ODPP jana.
Tukio hilo la mauaji lililotokea Oktoba mwaka jana limekuwa likichunguzwa na maafisa wa uchunguzi wa jinai kubaini waliohusika na waliochochea ghasia hizo zilizopelekea Gumbao Jola kuuawa.

Kwa muda wa mwaka polisi wamekuwa wakichunguza iwapo mbunge huyo alikaidi sheria za uchanguzi na vile kubaini kuhusika kwake katika mauaji hayo.

Bi Jumwa, anayeelezwa na upande wa mashtaka kuwa mbishi na mchochezi adaiwa alivamia boma la Bw Katana akiandamana na wafuasi wake ambapo ghasia zilichipuka..

Bw Jola alipigwa risasi katika eneo la Mshongaleni Pendu Kian iliyoko kaunti ya Kilifi.

Wafuasi zaidi ya 500 ODM walikuwa wameuhudhuria mkutano wa kuweke mikakati ya uchaguzi mdogo uliokuwa unaandaliwa.

You can share this post!

Hofu ya wimbi la pili la maambukizi ya corona

Kibarua cha kuokoa UhuRuto