Wanafunzi waliokataa kurudi shuleni wasakwa na machifu
Na Wycliffe Nyaberi
MACHIFU na maafisa wa Nyumba Kumi katika eneo la Nyamagwa, Kaunti ya Kisii, wameanzisha msako wa kuwatafuta wanafunzi ambao bado hawajarejea shuleni.
Kwa kuwa wanafunzi walisalia nyumbani muda mrefu kufuatia mkurupuko wa ugonjwa wa visrusi vya corona, wanafunzi wengi walikoma kudurusu na kujiingiza katika kazi za kujitafutia hela za haraka.
Baadhi ya wavulana walikimbilia kuendesha bodaboda na wasichana wengine wakajitosa kwenye starehe zilizowapelekea kutungwa mimba za mapema.
Hata hivyo, licha ya utundu huo, wazazi kwa ushirikiano na machifu katika eneo la Nyamagwa wameahidi kushirikiana ili wahakikishe hakuna mwanafunzi anayekatiza masomo yake licha ya changamoto zilizowapata. Wakiongozwa na chifu wao Bw Donald Aiko, wazazi hao wameapa kuwatafuta wanafunzi ambao bado hawajaripoti shuleni na kujua sababu zinazowafanya kutoendeleza masomo yao.
Kwa kuwa serikali inajitahidi kuimarisha miundomsingi na kuweka rasilimali ili kufadhili masomo, wazazi hao wanawataka watoto wote wanufaike na mpango huo.
“Tumekuwa tukiomba serikali iweze kufungua shule na imefanya hivyo. Basi mbona tuendelee kuwaweka watoto wetu nje ilhali tumekuwa tukitamani shule zifunguliwe?”Akauliza chifu Aiko.
Kwa wanafunzi waliopachikwa mimba wakiwa nyumbani, chifu huyo amewaomba wazazi kuwatia moyo warejee shuleni hadi watakapokaribia kujifungua.
Isitoshe, onyo kali limetolewa kwa wamiliki wa bodaboda ambao huwapa watoto wavulana pikipiki ili wafanye biashara nazo. Sasa afisa huyo amesema watanasa pikipiki zinazoendeshwa na wanafunzi na wenyewe kuchukuliwa hatua.