Habari Mseto

Shule 11 zahamishia wanafunzi kwingine

October 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

SHABAN MAKOKHA na LIZ OJINA

SHULE 11 zimekosa kufunguliwa baada ya kuharibiwa na mafuriko katika maeneo ya Magharibi na Nyanza.

Katika eneo la Budalang’i, Kaunti ya Busia, wanafunzi wa shule tano wamelazimika kuhamishiwa shule jirani baada ya vyoo na madarasa kuharibiwa na maji.

Shule zilizoharibiwa ni shule ya wanafunzi wa mahitaji maalumu ya Rugunga, shule ya msingi ya Buongo, shule ya upili ya Musoma, shule ya msingi ya Musoma ACK na shule ya msingi ya Igigo.

Mafuriko hayo yalitokea baada ya Mto Nzoia kuvunja kingo zake na kusababisha maelfu ya watu kupoteza makazi na mali yao.

Mkurugenzi wa elimu ukanda wa Magharibi Stephen Barongo alisema wanafunzi wa shule zilizoathiriwa na maji wamehamishiwa katika shule jirani za umma.

Bw Barongo alisema kuwa wanafunzi wa Gredi 4, Darasa la Nane na Kidato cha Nne wamekuwa wakisomea katika shule jirani tangu Jumatatu. Wizara ya Elimu imehamishia wanafunzi wa shule ya msingi ya Igigo katika shule ya msingi ya Budalang’i huku wenzao wa Musoma ACK wakipelekwa Rugunga.

Wanafunzi wa shule ya watoto wenye mahitaji maalumu ya Rugunga wamepelekwa katika shule ya Lugale na wenzao wa shule ya msingi ya Buongo wamehamishiwa Mubwayo.

Wanafunzi wa shule ya upili ya Musoma sasa wanasomea katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Sango.

Bw Barongo alisema kuwa shule zilizotumiwa kama kambi ya waathiriwa wa mafuriko tayari zimenyunyiziwa dawa na ni salama kwa wanafunzi.

Serikali ilifunga shule na vyuo mara baada ya kisa cha kwanza cha mwathiriwa wa virusi vya corona kuthibitishwa humu nchini mnamo Machi, mwaka huu.

Wanafunzi wa Gredi 4, Darasa la Nane na Kidato cha Nne walirejea shuleni Jumatatu huku wizara ya Elimu ikiwataka wanafunzi wa madarasa mengine kujiandaa kwa ajili ya ufunguzi wa shule wakati wowote.

Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Busia Florence Mutua aliitaka serikali kukarabati shule zilizoathiriwa na mafuriko kabla ya wanafunzi wengine kuruhusiwa kurejea shuleni.

Katika eneo la Nyando, shule sita ziliharibiwa na mafuriko, kulingana na Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti ya Kisumu Isaac Atebe.

Wanafunzi wa shule ya msingi ya Kandaria wamehamishiwa katika shule ya msingi ya Ugwe.

Wanafunzi wa shule ya upili ya Ombaka sasa wanasomea katika shule ya msingi ya Ombaka huku wenzao wa shule ya upili ya Kandaria wakihamishiwa katika shule ya upili ya Nduru. Mkurugenzi wa Tume yaHuduma kwa Walimu wa Kaunti ya Kisumu Ibrahim Rugut alisema kuwa walimu wa shule zilizoathiriwa pia watapelekwa katika shule ambazo wanafunzi wao wamehamia.

“Tutahamisha walimu wa shule zilizoathiriwa ili wafuate wanafunzi wao,” akasema.