• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Wanawake wangali nyuma kimaendeleo – Ripoti

Wanawake wangali nyuma kimaendeleo – Ripoti

Na MASHIRIKA

IMEBAINIKA kuwa ni karibu thuluthi moja pekee ya wanawake nchini wanaoweza kushiriki kikamilifu katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni. Kwa mujibu wa utafiti huo, uliofanywa na Mpango wa Kuwainua Wanawake Kenya (WEI), ilibainika ushiriki wao huathiriwa na hali na mazingira wanayokumbana nayo.

Hili linajiri huku dunia nzima ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Wanaoishi Maeneo ya Mashambani.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Kuimarisha hali za wanawake wanaoishi maeneo ya mashambani wakati wa janga la virusi vya corona.”

Mpango huo, ambao huendeshwa kwa pamoja na Halmashauri ya Kukusanya Takwimu Kenya (KNBS), Idara ya Masuala ya Jinsia, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Masuala ya Wanawake (UN Women) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Masuala ya Watoto (UNICEF), huwa unatoa takwimu za kina kuhusu mikakati ya kuboresha hali ya wasichana nchini.

Kwa mujibu wa utafiti huo, hali za karibu nusu ya wanawake wanaoishi maeneo ya mijini zimeboreka ikilinganishwa na wenzao katika maeneo ya mashambani, ambapo ni robo pekee hali zao zimeboreka.

Katika makazi ambapo wanaume wana elimu ya kiwango cha shule ya upili, hali za wanawake zimeboreka mara nne zaidi ikilinganishwa na makazi ambayo wanaume hawana kiwango chochote cha elimu.

Katika makazi ambapo mwanamume amepata elimu ya chuo anuwai ama chuo kikuu, hali za wanawake zimeboreka mara sita zaidi ikilinganishwa na makazi ambapo mwanamume hana kiwango chochote cha elimu.

Katika maeneo yenye kiwango cha juu cha umaskini, wanawake hukumbwa na ugumu mkubwa kufanya maamuzi huru.

Kwa mujibu wa utafiti huo, ni wanawake saba pekee kati ya mia moja katika maeneo hayo ambapo hali zao zinaweza kuboreshwa ikilinganishwa na zaidi ya nusu katika maeneo tajiri.

Masuala mengine yaliyotajwa kuchangia kiwango cha uboreshaji wa hali ya mwanamke ni hali yake ya ndoa.

Kwenye taarifa jana, Umoja wa Mataifa (UN) uliwasifu wanawake hao, ukisema huwa wanatekeleza majukumu muhimu katika ustawishaji wa jamii.

“Wanawake huwa wanatekeleza majukumu mazito katika mazingira magumu sana. Wengi hukumbwa na changamoto kubwa za ukosefu wa mahitaji na huduma za kimsingi kama maji na chakula,” ikasema UN.

Nchini India, mamia ya wanawake wamebuni makundi ya kujiinua kiuchumi, ambayo yamekuwa yakishiriki kwenye katika kutengeneza barakoa, sanitaiza na uuzaji chakula, hasa wakati huu dunia inakumbwa na janga la corona.

Nchini China, wanawake wamebuni vyama vya ushirika kuisaidia serikali kwenye mikakati ya kudhibiti corona. Mikakati kama hiyo inaendeshwa na wanawake katika nchi za Mali na Senegal.

You can share this post!

Shule 11 zahamishia wanafunzi kwingine

AFYA: Ngoja ngoja ya miezi tisa kaja na majonzi tele