• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
Wachonyi walia mradi wa utamaduni kucheleweshwa

Wachonyi walia mradi wa utamaduni kucheleweshwa

Na MAUREEN ONGALA 

KWA umbali unapokaribia ofisi ya Naibu Kamishina wa Chonyi iliyo katika kata ya Bandarasalama eneo bunge la Kilifi Kusini, utavutiwa na  jengo kubwa la kifahari  lenye mabati  mekundu na ukuta wa mawe  uliopakwa rangi nyeupe, na pia madirisha makubwa yenye vioo. 

Lakini unapofika karibu na jumba lile, utakaribishwa  na popo walioning’inia juu ya dari, milango iliyovunjika na kwenye sakafu ni vumbi na kinyesi cha wanyama hao, ishara kuwa halitumiki.

Hilo ndilo jumba ambalo lingebadilisha maisha ya wenyeji na kuinua kiuchumi jamii ya Chonyi ambayo ni mojawapo ya makabila tisa ya Mijikenda katika eneo la Pwani.

Hata hivyo wenyeji hao  huenda wakasubiri kwa muda mrefu  kabla ya kuanza kutumia  jumba hilo ambalo lilikusudiwa kuwa  mahali pa kudumisha na kuhifadhi  mila na desturi  za jamii hiyo, baada ya ujenzi wa jengo hilo kutokamilika miaka minane tangu ianze kujengwa.

Mradi huo  ulianzishwa na serikali kuu kupitia Wizara ya Utamaduni na Huduma za Jamii  mwaka wa 2012 muda mfupi kabla kuwepo kwa serikali za ugatuzi , baadae  waliukabidhi rasmi kaunti ya Kilifi mwaka ya 2015 ili waweze kuumaliza na kutumia kwa manufaa ya jamii.

Baada ya ya kukabidhiwa mradi huu, wawakilishi wa wadi katika bunge la kaunti ya Kilifi walitengeneza mpango ambao ulifanya chumba hicho kutumika kwa matumizi mbalimbali, mbali na kuwa kituo cha kuwavutia watalii na kile cha kuhifadhi  na kudumisha  mila na destruri za jamii ya Chonyi.

Ili kukamilisha mradi huo, walitenga Sh26 millioni. Hata hivyo, viongozi mbalimbali kutoka katika jamii ya Chonyi wakiongozwa na mbunge wa eneo bunge la Kilifi Kusini, Bw Ken Chonga walieleza masikitiko yao kwa jinsi mradi huo umecheleweshwa.

Chonga alisema kuwa mradi huu ni muhimu sana kwa kuongeza dhamana katika mila na destruri za jamii hiyo.

“Tunataka kufufua mila za Wachonyi ambazo zimesahaulika na pia kuna vigango ambavyo wazee wa  jamii yetu walikuwa wanavitumia kufanyia matambiko au kwa sherehe na ambavyo vinazidi kupotea, kwa kuwa vizazi vyetu hawavifahamu,”akasema. 

Mbunge huyo alisema kuwa katika historia ya Mijikenda, watu wengi hawajui kwamba kuna makabila mengine bali wanafahamu tu kabila la Giriama na Digo.

“Mpangilio huu ni mzuri kwa kuelimisha umma na vizazi vingine kuhusu makabila tisa ya Mijikenda na pia historia ndefu ya jamii ya  Chonyi  tokea mwanzo hadi sasa.,”akaongeza kusema.

Alikosoa kuzembea kwa kaunti ya Kilifi kukamilisha mradi huo wa mamilioni ya pesa na kusema kuwa ni uvujaji wa pesa ya umma.

Bw Chonga aliwahimiza wahusika kukamilisha mradi huo kwa haraka.  “Kaunti ya Kilifi iweze kukumbuka mradi huu na kuangalia ni jambo lipi ambalo halijakamilika na kutekeleza kwa haraka kwa manufaa ya jamii,” akasema.

Aliyekuwa mwakilishi wa wadi ya Mwarakaya Daktari Silas Chitibwi alisema kuwa mradi huo ulichukua miaka mitatu kujengwa baada ya kupokelewa kutoka kwa serikali kuu, na alishangaa ni kwa nini haujaanza kutumika.

Bw Chitibwi alisema kuwa baada ya ujenzi wa jumba hilo kukamilika, kungeteuliwa kamati ya usimamizi au bodi itakayoendesha shughuli zote zitakokuwa zinaendelea.

“Ujenzi wa chumba hiki ulikamilika miaka mitatu tu baada ya serikali ya kaunti kuidhinisha pesa lakini sijui tatizo liko wapi kwani mpaka sasa bado ndani hakujawekwa vifaa vvovvote na viti pia hakuna. Kamati iliyokuwa imependekezwa kusimamia shughuli zote zitakazoendelea hapo ilikuwa na jukumu la kutengeneza ziara ambapo wangewahamasisha wananchi kutoka kaunti mbalimbali kuhusu mila zao, jambo ambalo lingechagia kupanua eneo la Chonyi kimaendeleo” akasema.

Aliongeza kusema kuwa kwa miaka mingi sasa eneo la Chonyi halijaweza kuwa na maendelo ya kiuchumu hali ambayo imechangiwa na ukosefu wa miradi ya maendeleo ikiwemo viwanda.

Kulingana na kiongozi huyo, kuanza kutumika kwa jumba hilo ni hatua moja ya kuinua sehemu hiyo kiuchumu.

Chitibwi alisema kuwa inasikitisha kwamba hadi sasa wachonyi hawajaweza kufaidika na mradi huo.

“Lengo kuu la mradi huu lilikuwa liwe na kituo cha kuhifadhi na kuendeleza mila na tamaduni za Wachonyi na pia kituo cha kuvutia watalii ambacho kinafaa kujumuisha studio za kurekodi, bila shaka tungekuwa na  sehemu maaalum  ya makumbusho  ikiwemo mabakio ya vifaa vya kihistoria na maktaba  yetu. Yaweza kuwa changamoto ya fedha ilichangia kukawawia kwa mradi huu kumalizika, lakini kwa sasa siwezi nikaeleza ni nini kinachoendelea kwa sababu jengo liko tayari bado vifaa tu,”akasema. 

Kiongozi huyo alisema kuwa mtu yeyote asiyetoka katika jamii ya Chonyi anaweza kupuuzilia mbali mradi huu, lakini kwa jamii hiyo, ilikuwa ni chanzo cha mwamko mpya.

“Hatujarekodi mila na desturi ya Wachonyi, hata historia. Yote haya yamebakia tu kumbukumbu miongoni mwa wazee wetu, hata lugha yetu ya Chonyi inazidi kudidimia sasa na kuna vizazi ambavyo havijaweza kujua lugha hii kwa undani,” akasema.

Kabla ya kuhamishwa hadi idara ya maswala ya ardhi, waziri wa maswala ya jinsia na huduma ya jamii na michezo katika kaunti ya Kilifi, Bi Maureen Mwangovya alisema kuwa mradi huo haujaanza kutumika kwa sababu haujakabidhiwa rasmi kwa kaunti hiyo.

Katika bajeti ya mwaka 2018/2019 kaunti ya Kilifi iletenga Sh4 millioni kwa minajili ya kumalizia jengo hilo na Sh1.5 milioni ya kurembesha mazingira ya jumba hilo.

Tarehe 15 Mei 2019, Idara ya Jinsia, Huduma za Jamii na Michezo ilitangaza tena kandarasi ya kuweka vifaa katika jumba hilo ikiwemo chumba cha filamu.

Kwa sasa jumba hilo linatumika kama sehemu ya kufanya mikutano japokuwa hamna viti wala vipaza sauti.

You can share this post!

WALLAH: Umoja huwa nguvu imara kuliko nguvu za kutumia kifua

Maporomoko yazua huzuni Pokot