Habari Mseto

Wataka wa Kakuzi wataka vikao vya wazi kukusanya ushahidi kuhudu dhuluma

October 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

Wakazi wanaoishi karibu na kampuni ya Kakuzi, Kaunti ya Murang’a sasa wanataka mahakama ya wazi ibuniwe kupokea ushahidi kutoka kwa watu kufuatia madai ya ukiukaji wa haki zao na wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Mnamo Jumapili gazeti la Uingereza la Sunday Times liliripoti kuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo wakiwemo walinzi wamekuwa wakiwapiga, kuwabaka, kuua na kujeruhi watu wanaoishi karibu na mashamba yake kwa zaidi ya mwongo mmoja uliopita.

Kulingana na mwenyekiti wa chama cha wakazi wa eneo la Kandara, Bw Philip Kamau, ni kupitia mikutano ya wazi, inayoandaliwa na serikali, watetezi wa haki za binadamu, mawakili wa jamii na wanasheria inayoweza kupata ukweli.

Bw Kamau alisema mzozo wa sasa hauwezi kutatuliwa kwa kubadilisha taarifa za kuunga au kupinga madai yaliyofanya kampuni hiyo kushtakiwa katika mahakama ya Uingereza bali ni kwa kupitia mikutano ya ukweli, haki na maridhiano.

Alisema kwa kampuni ya kigeni kulaumiwa kwa mauaji, ubakaji, unajisi miongoni mwa maovu mengine sio jambo linaloweza kuachwa kupita, kwa kukusanya taarifa za kuunga na kupinga ilivyofanyika mara nyingi kampuni hiyo ilipolaumiwa kwa maovu.

Alisema kwamba kampuni hiyo imeajiri zaidi ya wafanyakazi 3000, inalipa kodi, imeorodheshwa katika soko la hisa na kwamba huwa inanunua tani 600 za avokado haziwezi kulinganishwa na katiba inayotambua haki za binadamu ambazo imedaiwa kukiuka.

Wakili Timothy Mwangi ambaye ni afisa wa tawi la Murang’a la chama cha wanasheria nchini (LSK) alisema kwamba kuna kesi kuhusu vitendo vya Kakuzi kortini na masuala yote yaliyo katika karatasi la mashtaka yataamuliwa kwa kuzingatia uzito wake.

Seneta wa Murang’a, Bw Irungu Kang’ata, jana aliambia Taifa Leo kwamba habari za vyombo vya habari kuhusu masaibu ya Kakuzi zitaathiri wakulima wa avokado. Alisema kwamba waathiriwa wa madai ya ukatili wa kampuni hiyo wanafaa kutendewa haki.

“Lakini hii haifai kufanya sekta ya avokado kaunti ya Murang’a kuvurugika. Soko halifai kuhusishwa katika kesi,” alisema.

Bw Kang’ata anasema wakulima wa kaunti hiyo waligeukia kilimo cha avokado baada ya sekta ya Kahawa na majani chai kuvurugika miongo miwili iliyopita na mzozo wa Kakuzi haufai kuwaharibia soko.

Tayari, kampuni iliyokuwa ikinunua avokado nchini Uingereza. Tesco Supermarket, imesimamisha Kakuzi hadi uchunguzi unaoendelea na kesi iliyo kortini itakapokamilika.

Mwenyekiti wa shirika la Murang’a Human Dignity Lobby Group,Keith Mureithi, alisema hawatakubali haki zao zikiukwe ili kulinda maslahi ya kibiashara. Alisema madai dhidi ya Kakuzi ni mabaya sana.