RAMADHANI: Saumu huwakinga wanaofunga dhidi ya maasia na machafu
Na KHAMIS MOHAMED
FUNGA ni Kinga. Ni kinga itakayo kinga Mja na moto wa jahanamu, itamkinga mwenye kufunga dhidi ya madhambi, maovu na machafu.
Ni maumbile ya nafsi ya mwanadamu kupenda mno kutenda maovu kama alivyosema Mwenyezi Mungu “…kwa hakika (kila) nafsi ni yenye kuamrisha sana maovu, isipokuwa ile ambayo mola wangu ameirehemu…” [12:53]
Funga iliyokamilika inamlinda na maradhi mbali mbali katika mwili wake na maradhi ya nafsi yake.
Ndipo Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad rehema na amani zimshukie alisema akiwaelezea kundi la vijana jinsi ya kuyavunja na kuyazima matamanio kwa kutumia silaha ya swaumu, akasema:
“Enyi kusanyiko la vijana! Yeyote miongoni mwenu atakayeweza kuoa basi na aoe, kwani huko (kuoa) kunalihifadhi mno jicho na kunaipa ngome tupu. Na asiyeweza (gharama za ndoa), basi na ajilazimishe na swaumu, kwani hiyo (swaumu) ni kinga kwake (dhidi ya maasi)”. Bukhaari na Muslim.
Na ni kweli kabisa aliyoyasema Bwana Mtume, kwani imethibiti kupitia majaribio kwamba swaumu inapunguza matamanio kwa kiwango kikubwa sana, kama sio kuyakata kabisa.
Mtume wa Mwenyezi Mungu Rehama na Amani zimshukie-amesema: “…na swaumu ni kinga, atakapofunga mmoja wenu asiseme maneno machafu siku hiyo na wala asipayuke. Iwapo mtu atamtukana au kumpiga, basi na aseme hakika mimi nimefunga”. (Muslim).
Mfungaji kukatazwa kusema maneno machafu na kupayukapayuka ovyo, kuna msaada mkubwa kwake katika kuidhibiti nafsi yake; ulimi, viungo na moyo wake dhidi ya kutenda maasi.
Mojawapo ya mambo yatakayokusaidia kuihepa adhabu kali ya moto ni ibada ya swaumu. Kama alivyosema Mtume wa Mwenyezi Mungu Rehema na Amani zimshukie: “Swaumu ni kinga na ni ngome madhubuti dhidi ya (adhabu ya) moto”. (Ahmad).
Hali kadhalika, Allah huwaneemesha baadhi ya wafungaji kwa kuwaacha huru na adhabu ya moto kama alivyosema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Hakika Allah Taala anao waachwa huru na moto wakati wa kila kufuturu na hilo (hupatikana) katika kila usiku”. (Ahmad).
Kama tuonavyo funga ni kinga tosha kutokamana na maasi na machafu iliyobaaki ni kila aliyefunga anatakiwa kuzidisha ibada kwa maneno na vitendo. Walioghafilika huko nyuma wazinduke na kuifanye Ramadhani hii kama kitu cha kuwabadilisha.
Walete toba kwa wingi, wasimame sana usiku kwa kufanya ibada na kumtaja sana Mwenyezi Mungu kwa sababu huu ndio mwezi wa kuchuma thawabu kwa wingi bila masumbuko ya nafsi ama shetani kwani wote washafungwa minyororo.
Mwenyezi Mungu atuepushe na moto wake.