Wanasiasa wanaozindua miradi hewa wakaangwa mitandaoni

NA PETER MBURU

WAKENYA mitandaoni wamewakaanga bila mafuta baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa na hulka ya kuzindua miradi isiyo na mashiko na kuitumia kusaka umaarufu.

Hii ni baada ya tabia miongoni mwa baadhi ya viongozi kuibuka, ambapo wanaidhinisha miradi yenye mabadiliko finyu kwa maisha ya wananchi, lakini kuitumia kutafuta sifa kwa udi na uvumba.

Baadhi ya wanasiasa hutumia kila mbinu kulipua miradi midogo iwe na sura ya ukubwa wa manufaa, na hata wanapotaka kutokea kwenye vyombo vya habari kujaribu njia zote za kuitafutia picha mwafaka.

Kati ya viongozi ambao wamejipata kwenye kurunzi ya wakenya ni mbunge wa Nandi Hills Alfred Keter (pichani juu) na naibu gavana wa kaunti ya Nakuru Dkt Eric Korir.

Naibu gavana wa Nakuru Dkt Eric Korir akizindua viti katika hafla ya hivi majuzi. Picha/ Peter Mburu

Kwenye picha zilizoko mitandaoni, wawili hao wanaonekana wakizindua miradi, japo wakenya wakizidiwa na maswali kuhusu umuhimu wa picha katika miradi hiyo.

Bw Keter, ambaye alibanduliwa kutoka kiti cha ubunge na mahakama ya Eldoret anaonekana akizindua tanki mbili za maji, ilhali Bw Korir naye anazindua viti.

Picha hizi zimeibua ucheshi, na pia kukosolewa na watumizi wa mitandao ambao wanahisi viongozi hawa ‘wamekuja sana’.

“Kazi zingine ni za MCA, hawa viongozi wamezidi pia,” akasema mtumizi mmoja wa Facebook, akiungwa mkono na wengi.