Waititu kupimwa corona kabla ya kushtakiwa
Na RICHARD MUNGUTI
HAKIMU anayesikiza kesi ya ufisadi inayomkabili Ferdinand Waititu ya Sh598milioni aliamuru apimwe katika hospitali ya serikali kubaini ikiwa amepona ugonjwa wa corona.
Hakimu mwandamizi Bw Thomas Muthoka aliamuru afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma achunguze na kubaini aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu ni mgonjwa.
Bw Waititu aliyekuwa ameambukizwa ugonjwa wa Corona hakufika kortini jana wakati wa kusikizwa kwa kesi ya ulaghai wa zaidi ya Sh598milioni.
Hakimu alifahamishwa na wakili John Swaka kwamba gavana huyo wa zamani anayeshtakiwa pamoja na mkewe Susan, ni mgonjwa.
Kiongozi wa mashtaka Bw Victor Mule alielezea tashwishi kuhusu ripoti iliyowasilishwa kortini “ikidai Bw Waititu amepewa muda wa siku saba apumzike.”
“Hii kesi lazima iendelee Oktoba 26, 2020. Imekawia hapa kortini kwa muda mrefu pasi kuanza,” alisema Bw Muthoka , huku , “ akiamuru afisa anayechunguza kesi achunguze na kuthibitisha ikiwa ripoti iliyotolewa na hospitali ya Super Care Center ni sahihi kwamba Bw Waititu ni mgonjwa.”
Wakili John Swaka aliwasilisha barua kutoka kwa hospitali ya Super Medical Center ikisema “ Waititu apumzike kwa siku saba.”
Gavana huyu wa zamani alikuwa amepimwa Corona katika kiliniki cha Lancer na kupatikana ameambukizwa.