• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 5:55 AM
BBI yapendekeza tume ya afya ya akili

BBI yapendekeza tume ya afya ya akili

Na CHARLES WASONGA

RIPOTI ya Mpango wa Maridhiano (BBI) imependekeza kuundwa kwa Tume ya Afya ya Akili na Furaha (Mental Health and Happiness Commission) kutokana na sheria mpya kuhusu afya ya akili itakayoshughulikia visa vingi vya maradhi ya kiakili ambayo yanaongezeka kila siku nchini.

Kwenye mapendekezo yaliyowasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga mjini Kisii kamati maalum kuhusu BBI ilisema kwamba pendekezo hilo ni miongoni mwa masuala yaliyoibuliwa na jopokazi lililoteuliwa 2019.

Mapendekezo ya jopokazi hilo yanalenga kushughulikia visa vya afya ya kiakili nchini.

“Wadau walipendekeza hatua ambazo serikali inastahili kuchukua kupunguza madhila ya waathiriwa wa maradhi hayo na jamaa zao,” ripoti ya jopokazi hilo ilisema.

Ikaongeza: “Mapendekezo hayo yanayojumuisha uundaji wa sheria kuhusu afya ya akili itakayopelekea kuundwa kwa Tume ya Afya ya Kiakili na Furaha.”

Jopokazi hili lililoongozwa na mtaalamu wa masuala ya afya ya akili Dkt Frank Njenga lilibuniwa kufuatia hatua ya Rais kutangaza tahadhari kuhusu kupanda kwa visa vya maradhi ya kiakili nchini Kenya.

Jopokazi hili lilitwikwa jukumu la kusaka njia ya kuwezesha waathiriwa kupata matibabu na aina zingine za usaidizi; na kupunguza unyanyapaa unaowakumba wagonjwa hao.

Dkt Njenga na wenzake pia walipaswa kutafutia njia za kuwasaidia watu ambao huwatunza waathiriwa wa maradhi ya akili.

Katika mapendekezo yake kamati ya maridhiano iliyooongozwa na Seneta wa Garissa Yusuf Haji inapendekeza kuongezwa kwa ufadhili kwa huduma za afya ya akili katika ngazi za serikali kuu na zile za kaunti.

Ripoti ya BBI pia inapendekeza kuharakishwa kwa uundwaji wa Mswada kuhusu Watu wanaoishi na Ulemavu na utayarishaji wa mikakati ya kutathimi viwango vya furaha miongoni mwa wananchi ni (National Happiness Index).

Kando na hayo ikiwa ripoti ya BBI itapitishwa, serikali za kaunti zitahitajika kuunda sera, maongozi na sheria za kudhibiti matumizi ya mihadarati na pombe.

You can share this post!

TAHARIRI: Kila mtu asome BBI bila shinikizo

NGILA: Tusipochunga, taka za kielektroniki zitatuumiza