Madaktari watatu kumpima Waititu
Na RICHARD MUNGUTI
MKURUGENZI wa mashtaka ya umma (DPP) Jumatatu aliomba mahakama iamuru Bodi ya Madaktari (KMPDB) iteue madktari watatu kumpima aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu Baba Yao kubaini ugonjwa anaougua.
DPP kupitia kwa naibu wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma DDPP Victor Mule aliomba korti iamuru KMPDB iteue madaktari kumfanyia ukaguzi Bw Waititu ambaye amekosa kufika kortini wakati wa kusikizwa kwa kesi inayomkabili ya kupokea mlungula wa Sh510m.
Mahakama ilifahamishwa na wakili John Swaka kwamba Bw Waititu angelifika kortini kwa vile ameambukizwa ugonjwa wa Covid-19.
Bw Mule anayesaidiana na mawakili waengine wanne wa serikali walimweleza hakimu mwandamizi Bw Thomas Muthoka kwamba kutofika kortini kwa Bw Waititu kumeathiri kusikizwa kwa kesi inayomkabili , mkewe Susan na washtakiwa wengine waliokuwa wafanyakazi wa kaunti hiyo ya Kiambu.
“Tabia hii ya Bw Waititu imeathiri kusikizwa kwa kesi inayomkabili yeye na washtakiwa wengine.Naomba korti iendelee na kesi hii bila Waititu,” Bw Mule alieleza Bw Muthoka.
Lakini Bw Swaka alipinga ombi hilo la DPP akisema afya ya mshukiwa ni muhimu na kamwe hapasi kushurutishwa kuendelea na kesi ilhali akiwa sio buheri wa afya.
Bw Muthoka atatoa uamuzi Oktoba 28 ikiwa kesi itaendelea bila Bw Waititu au la.