Tangatanga wadai BBI itampa Rais mamlaka ya kidikteta

Na SHABAN MAKOKHA

WABUNGE wa mrengo wa Tangatanga sasa wanaikosoa ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI) wakidai kuwa inampa Rais mamlaka makuu katika uteuzi wa Waziri Mkuu na manaibu wake wawili.

Wabunge hao Didmus Barasa (Kimilili), Justus Murunga (Matungu) na Kimani Ichungwa (Kikuyu) wanasema kuwa pendekezo hilo linarejesha mfumo mseto wa utawala wenye rais aliye na mamlaka zaidi kutofauti na hali ilivyo sasa.

Wanadai kuwa jopokazi la BBI limelirejesha taifa hili katika enzi za utawala wa kidikteta ulioshuhudiwa wakati wa utawala wa KANU chini ya Rais wa zamani marehemu Daniel Moi.

Wakenya waliidhinisha katiba ya sasa mnamo 2010 na kubadilisha mfumo wa utawala kutoka ule wa ubunge hadi ule wa urais, ambapo rais anachaguliwa pamoja na mgombeaji mwenza wake katika uchaguzi mkuu.

Ingawa BBI inalenga kuhakikisha kuwa watu wengi zaidi wanajumuisha katika utawala wa nchi, wabunge hao watatu wanataka Naibu Rais, Waziri Mkuu na manaibu wake waili wachaguliwe moja kwa moja na wananchi katika uchaguzi mkuu.

Mbw Barasa, Murunga na Ichungwa walisema ikiwa washikilizi wa nyadhifa hizi watachaguliwa na Rais, afisi hizo zitawajibika kwa Kiongozi wa Taifa na hivyo watafeli kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Endapo mapendekezo ya BBI yatapitishwa, waziri mkuu atakuwa mbunge ambaye atateuliwa kutoka chama au muungano wenye wabunge wengi katika bunge la kitaifa.

Atakuwa kiongozi wa shughuli za serikali bungeni katika bunge la kitaifa ambaye atashirikisha majukumu ya Wizara na Idara za Serikali.

Anaweza kufutwa na Rais au aondelewe kupitia kura ya kutokuwa na imani naye bungeni. Manaibu wawili wa Waziri Mkuu watachaguliwa na Rais kutoka miongoni mwa Mawaziri.

“Sio vizuri kwa nchi kuwa na kiongozi mmoja mwenye mamlaka makuu kuliko wengine. Tunafaa kusambaza mamlaka kupitia uchaguzi ili hamna mmoja anayeendeleza masilahi ya mwingine,” akasema Bw Ichungwa ambaye walikuwa wameandamana na Naibu Rais William Ruto kwa mchango katika eneo bunge la Matungu Jumapili.

Habari zinazohusiana na hii

Kwa nini tunapinga BBI

Hisia mseto kuhusu BBI