• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
Rigathi Gachagua ahojiwa na DCI kuhusiana na sakata ya Sh12.5 bilioni

Rigathi Gachagua ahojiwa na DCI kuhusiana na sakata ya Sh12.5 bilioni

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Mathira, Rigathi Gachagua Jumatatu alihojiwa na maafisa wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kuhusiana na sakata ya Sh12.5 bilioni.

Bw Gachagua alifikishwa katika makao makuu ya idara hiyo jijini Nairobi ambapo alihojiwa kwa zaidi ya saa mbili kuhusiana na madai ya wizi wa pesa za umma, kisha akaachiliwa.

Kulingana na DCI, kampuni 22 zinazomilikiwa na mbunge huyo zilifaidi kutokana pesa hizo kupitia zabuni zilizopewa kutoka serikali ya kitaifa na zile za kaunti kinyume cha sheria.

Haya yanajiri baada ya kubainika kuwa akaunti za Bw Gachagua za benki zilifungwa ili kutoa nafasi kwa wapelelezi kuchunguza chanzo cha fedha ambazo zilipitishwa kwa akaunti hizo.

Akaunti zilizofungwa zilikuwa na Sh202 milioni, Sh35 milioni, Sh165 milioni, Sh1.1 milioni na Sh700,000.

Mbunge huyo anashukiwa kutumia maafisa fulani wenye ushawishi kupata zabuni kutoka serikali kuu na serikali za kaunti kinyume cha sheria.

Wakati wa uchunguzi kuhusu sakata hiyo, wapelelezi walienda katika kaunti tano, mashirika ya serikali na afisi za Hazina ya Maendeleo ya Eneo Bunge (CDF) la Mathira.

Viongozi wengine wanaodaiwa kufaidi kutokana na fedha hizo na ambao wamekuwa wakichunguzwa na DCI ni aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, Seneta wa Meru Mithika Linturi na Diwani wa wadi ya Ruguru Karanja Muriuki.

Hata hivyo, Bw Gachagua amejitetea dhidi ya madai hayo akisema kuwa alipata pesa hizo kupitia “biashara halali”.

“Madai hayo hayana misingi yoyote. Nimekuwa mfanyabiashara tangu nilioondoka utumishi wa umma na pesa zangu ni halali. Najua kwamba nawindwa kwa kuwa mshirika wa Naibu Rais William Ruto,” akasema.

You can share this post!

Tangatanga wadai BBI itampa Rais mamlaka ya kidikteta

Uhuru na Raila warai Wakenya waunge mkono BBI