21 wauawa kwenye machafuko ya matokeo ya uchaguzi Guinea
NA AFP
JUMLA ya watu 21 wameuawa katika michafuko nchini Guinea kufuatia uchaguzi wa urais unaopingwa huku wajumbe wa kimataifa wakijaribu kutuliza taharuki katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
Vyombo vya habari nchini humo vilisema kuwa watu 21 wameuawa tangu Oktoba 19, akiwemo maafisa wa usalama – idadi ambayo imepunguzwa kwa watu sita ikilinganishwa na upinzani unaodai ni watu 27 walifariki.
Rais Alpha Conde, 82, alishinda uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali wa Oktoba 18 kulingana na matokeo rasmi yaliyotangazwa Jumamosi, na kuashiria mwanzo wa muhula wa tatu unaokumbwa na utata.
Mpinzani wake mkuu Cellou Dalein Diallo, 68, amepinga matokeo hayo.Alidai kuibuka mshindi wiki jana akinukuu data ambayo wanaharakati wake walinyakua katika vituo vya upigaji kura.
Hatua ya Diallo kujitangaza mshindi ilisababisha makabiliano makali yaliyodumu wiki moja.