• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 5:55 AM
BBI yazua mpasuko kisiasa

BBI yazua mpasuko kisiasa

Na WAANDISHI WETU

WANASIASA sasa wametofautiana kuhusu ikiwa ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) inastahili kufanyiwa marekebisho kwa mara nyingine.

Baadhi ya viongozi wamesema inastahili kuwepo nafasi ya marekebisho ili kujumuisha maoni ya wale wanaopinga yaliyomo, lakini wengine wanasema hakuna muda wa kuanza kupokea maoni upya.

Wakiongea jana asubuhi katika mahojiano ya runinga, wabunge Chris Wamalwa (Kiminini), Gladys Shollei (Mbunge Mwakilishi, Uasin Gishu) na Seneta Maalum Isaac Mwaura wanamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuteua kamati ndogo ya watu watano au saba kupiga msasa ripoti hiyo wakizingatia kauli zinazoibuliwa na Wakenya kuihusu.

‘Ripoti hii haipasi kupitiliwa mbali, lakini sehemu kadha ziboreshwe ili kuafiki matakwa ya Wakenya. Kazi hiyo ifanywe na kamati ndogo ya watu watano au sababu itakayojumuisha wawakilishi kutoka makundi ya kidini, Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) na makundi ya mashirika ya kijamii. Wanasiasa wasiwe wanachama wa kamati hiyo kwani watapata nafasi ya kuichambua bungeni,” akasema Bw Wamalwa, kauli ambayo iliungwa mkono na Shollei na Mwaura.

Watatu hao walisema ripoti hiyo halijatanzua suala la mshindi kutwaa kila kitu ambalo ndio husababisha ghasia kila baada ya chaguzi, wakisema nyadhifa tatu kuu bado zinaweza kuendea watu kutoka chama cha Rais.

“Yusuf Haji na wenzake wamefanya kazi yao sasa, tunamtaka rais kuteua kama nyingine ya watu wachache ipige msasa ripoti hiyo kwa mwezi mmoja kisha iwasilishe nakala itakayowasilishwa bungeni kwa mjadala,” akasema Shollei.

Hata hivyo, kauli hii ilipingwa na Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna ambaye alisema hakuna wakati wa kuanza kupiga msasa tena ripoti hiyo.

Kulingana na Bw Sifuna, kulikuwa na muda wa kutosha awali kwa wadau na wananchi kutoa maoni yao kwa jopo la BBI.Katika ukanda wa Pwani, magavana Hassan Joho (Mombasa) na mwenzake wa Kilifi Amason Kingi waliwataka Wakenya kuisoma ripoti kwa makini na kuijadili ili waweze kuilewa.

Bw Joho alitaka Wakenya kujadiliana kwa heshima kwani anaamini ripoti imebeba mapendekezo ambayo yataboresha uongozi wa nchi hii huku ikipalilia umoja na utangamano wa kitaifa.

“Huu ndio mwanzo wa safari ya umoja, uwiano, maridhiano na ugavi bora wa raslimali kwa maendeleo ya taifa,” akasema kupitia twitter.Gavana wa Kilifi naye alisifu BBI akisema ni muhimu hususan kwa ugatuzi akisisitiza kuwa suala la kuongeza fedha kwa serikali za kaunti linafaa kupigiwa upatu.

“BBI imeahidi kuimrisha ugatuzi, Wakenya wanafaa kuiunga mkono ili serikali za kaunti zipate pesa zaidi za kufadhili maendeleo mashinani,” alisisitiza.

Kwingineko, Mwenyekiti wa Muungano wa Makanisa Yaliyosajili Kenya (ARCK) Askofu Samuel Manyonyi Wellimo, jana alisema japo kanisa linaunga mkono mapendekezo kama vile kuongezwa kwa mgao wa fedha kwa kaunti, linahofia kuwa wananchi bado atabebeshwa mzigo mzito.

Alisema kanisa linataka uongozi wenye maafisa wachache ambao hawatakuwa mzigo kwa wananchi.

“Huku tukilenga kuhakikisha kuunda serikali jumuishi, tunafaa kuwa na maafisa wachache ambao serikali itamudu kugharimia bila kuumiza Wakenya,” akasema Askofu Wellimo akiwa Bungoma.

Ripoti za CHARLES WASONGA, WINNIE ATIENO na BRIAN OJAMAA

You can share this post!

Uchambuzi wa Kitabu ‘Mbio Kuhimiza Umoja wa...

BBI: Uhuru alimcheza Raila?