BBI: Uhuru alimcheza Raila?
Na WANDERI KAMAU
KAULI ya Rais Uhuru Kenyatta mnamo Jumatatu kuwa Naibu Rais William Ruto alifahamu kuhusu handisheki, imeibua maswali kuhusu iwapo kinara wa ODM, Raila Odinga amekuwa akiwahadaa Wakenya kuhusu makubaliano hayo.
Tangu mwafaka kati ya viongozi hao wawili mnamo Machi 2018, Bw Odinga na washirika wake wamekuwa wakidai Dkt Ruto hakushiriki wala hakufahamu lolote kuhusu mazungumzo kati yake na Rais Kenyatta.
“Tulikutana peke yetu na Rais Kenyatta. Hakukuwa na yeyote mwingine,” alisema Bw Odinga awali.
Lakini akihutubu katika Ukumbi wa Bomas jana kwenye uzinduzi wa ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) mnamo Jumatatu, Rais Kenyatta alisema Dkt Ruto alifahamu kuhusu mchakato huo, kwani hata alikuwa na wawakilishi katika jopokazi la BBI.
Rais pia alisisitiza kuwa Dkt Ruto alifahamu kila kitu kuhusu mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea kati yake na Bw Odinga.
“Ningetaka kumshukuru naibu wangu kwani katika mchakato huo wote nilimfahamisha kuhusu yale yaliyokuwa yakiendelea. Alikuwa sehemu ya walioshiriki kwenye utaratibu huo, kwani hata alinisaidia kuwateua baadhi ya wanachama wa jopo la BBI,” akaeleza Rais.
Kauli ya Bw Odinga pia inatofautiana na matamshi ya Dkt Ruto kuhusu handisheki, ambapo amekuwa akishikilia kuwa yeye na Rais Kenyatta ndio waliojadili kuhusu haja ya kurejesha uthabiti wa kisiasa nchini baada ya uchaguzi huo.“Kabla ya handisheki, tulijadili kwa kirefu na Rais Kenyatta kuhusu umuhimu wa uwepo wa utulivu wa kisiasa nchini,” akasema Dkt Ruto kwenye mahojiano
.Mwelekeo huo umeibua tashwishi kuhusu kauli za baadhi ya washirika wa karibu wa Bw Odinga kwamba handisheki ilikuwa makubaliano ya Rais Kenyatta na Bw Odinga pekee.
Kwa mujibu wa wadadisi, kuna uwezekano kauli hizo ndizo zimekuwa chanzo kikuu cha mvutano ambao umekuwepo kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto.
Upeo wa tofauti hizo ulikuwa kuondolewa kwa baadhi ya washirika wa Dkt Ruto kwenye uongozi wa nafasi muhimu kwenye Seneti na Bunge la Kitaifa.