Kenya itaziadhibu Facebook, Twitter na Google zikiuza data ya wananchi – Kassait
Na CHARLES WASONGA
AFISI mpya ya Kamishna wa Kulinda Data italinda maelezo kuhusu Wakenya yanayohifadhiwa na kampuni za kubwa za kiteknolojia kama vile Facebook, Twitter na Google, Immaculate Kassait ambaye ameteuliwa kushikilia wadhifa huo amewahakikishia wabunge.
Bi Kassait, ambaye kabla ya Rais Uhuru Kenyatta kumteua alikuwa Mkurugenzi wa kitengo cha kutoa elimu kwa wapiga kura katika Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), alitoa hakikisho hilo alipokuwa akipigwa msasa na Kamati ya Bunge kuhusu Mawasiliano Jumatano.
Alionya kuwa kampuni hizo, ambazo pia huendesha mitandao ya kijamii, zitaadhibiwa kwa mujibu wa sheria mpya kuhusu ulinzi wa data, endapo zitatumia vibaya data Kenya au Wakenya.
Sheria kuhusu ulinzi wa data iliyopitishwa Novemba mwaka jana imeweka masharti kuhusu namna data za watu binafsi zinaweza kuhifadhiwa na kutumika na asasi za umma na zile za serikali.
Kulingana na sheria hiyo Kamishna wa Data ana mamlaka ya kuchunguza visa mbalimbali vya matumizi mabaya ya data zilizohifadhiwa na kupendekeza adhabu kwa wale ambao watapatikana na hatia ya matumizi mabaya ya maelezo hayo.
Kwa mfano, mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kuingilia, kuvuga au kusambaza data kuhusu mtu yeyote, zinazohifadhiwa na asasi za umma au zile kibinafsi atatozwa faini isiyozidi Sh5 milioni, kifungo kwa miaka 10 gerezani au adhabu zote mbili.
“Sheria hii itatumika hata kwa kampuni za kimataifa zenye data kuhusu Kenya na Wakenya kama vile; Google, Twitter na Facebook. Zina wajibu wa kuhakikisha kuwa zinazingatia sheria za Kenya kuhusu data,” Bi Kassait akawaambia wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na Mbunge wa Marakwet Magharibi William Kisang.
Itakumbukwa kuwa mnamo 2018, kampuni ya Facebook iliungama kuwa maelezo ya kibinafsi ya watumizi wake 87 milioni huenda zilisambazwa kwa kampuni ya ushauri wa kisiasa wa Cambridge Analytica, kinyume cha sheria.
Kampuni hiyo hii (Cambridge Analytica) ilipata umaarufu nchini kwa kuhusika katika kampeni za Rais Uhuru Kenyatta kuelekea chaguzi za 2013 na 2017. Kampuni hiyo pia ilimsaidia Rais wa Amerika Donald Trump katika uchaguzi wa urais wa 2016 na akaibuka mshindi.
Bi Kassait aliwaambia wabunge kuwa Wakenya wako na haki ya kubadilisha maelezo yao ambayo yamehifadhiwa na asasa mbalimbali ili kuafiki matakwa yao nyakati fulani.
“Kwa mfano, ikiwa kampuni kama vile zile za mawasiliano zina maelezo yanayosema kuwa unahutumiwa kwa uhalifu fulani. Kisa baada asasi za uchunguzi kubaini kuwa aliwekelewa makosa hayo na kwamba hauna hatia, ni haki yako kuomba maelezo yanayosema kuwa wewe ni mhalifu yaondolewe,” akasema.
Aidha, Bi Kassait aliongeza kuwa chini ya Sheria kuhusu Ulinzi wa Data, Wakenya watakuwa huru kuhamisha maelezo yao kutoka shirika/kampuni moja hadi nyingine.
“Vile vile, unaweza kuuliza Google ikwambie maelezo kukusu ambayo imehifadhi, wapi na kama ni sahihi,” akafafanua.
Bi Kassaiti alisema endapo uteuzi wake utaidhinishwa, ataanzisha mwongozo ambao utahakikisha kuwa data zote za Wakenya, zikiwemo zile za Huduma Namba, zimewekwa salama.
Mwaka jana Mahakama Kuu ilisema ukosefu wa sheria madhubuti ndio kizingiti kwa serikali kufanikisha mpango wa usajili wa watu kidijitali, kufuatia hofu kwamba data za Wakenya hazitakuwa salama.
Ikiwa bunge la kitaifa litaidhinisha uteuzi wa Bi Kassait, atasimamia data zote kutoka kwa wananchi ambazo serikali inahifadhi.
Data hizo ni kama zile wananchi kuwasilisha wanapoomba vitambulisho vya kitaifa, Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF), Paspoti, leseni ya kuendesha magari, vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya mienendo mizuri, miongoni mwa stakabadhi nyinginezo.
Bi Kassait amewahi kuhudumu kama mkurugenzi wa usajili wa wapiga kura katika IEBC kwa miaka tisa kabla ya kuhamishwa hadi kitengo cha elimu kwa wapiga kura.
Katika uchaguzi wa 2017 yeye ni miongoni mwa maafisa wa IEBC waliolaumiwa na mrengo wa upinzani, NASA, kwa kushiriki wizi wa kura.