BBI: Raila aikosoa IEBC, asema 'refarenda itagharimu Kenya Sh2 bilioni pekee'
NA WANDERI KAMAU
KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amekosoa vikali kauli ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwamba itaigharimu Kenya Sh14 bilioni kuandaa kura ya maamuzi kuhusu BBI.
Mnamo Jumatano, Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, Hussein Marjan alisema walifikia kiwango hicho baada ya kukutana na kutathmini gharama na huduma zote ambazo zingehitajika.
Lakini kwenye taarifa kwa vyombo vya habari jana, Bw Odinga alishikilia pendekezo lake la awali kwamba zoezi hilo halipaswi kuigharimu nchi zaidi ya Sh2 bilioni.
Kiongozi huyo amekuwa akishinikiza mageuzi makubwa katika IEBC, akiitaja kuwa chanzo cha matatizo ya kisiasa ambayo yamekuwa yakiiandama nchi hii kwa muda mrefu.
Wiki iliyopita, mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati, alimlaumu vikali Bw Odinga kwa kushinikiza kuondolewa kwa makamishna wake waliobaki kama mojawapo ya mageuzi yaliyopendekezwa na ripoti ya BBI.