• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Corona: Seneti kubadili taratibu za kuendesha shughuli

Corona: Seneti kubadili taratibu za kuendesha shughuli

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Seneti linapanga kubadili ratiba ya kazi zake litakaporejelea vikao Jumanne wiki ijayo kufuatia ongezeko la visa vya maambukizi ya Covid-19 nchini.

Spika Kennneth Lusaka amesema kuwa mabadiliko hayo pia yatahusisha kupunguzwa kwa idadi ya maseneta watakaoruhusiwa katika ukumbi wa mjadala kwa wakati mmoja. Maseneta wengine watalazimika kufuatilia mijadala kwa njia ya mtandao.

“Seneti inarejelea vikao vyake wiki ijayo lakini kutokana na ongezeko la visa vya maambukizi tutalazimika kubadili taratibu za kuendesha shughuli zetu huku tukipunguza idadi ya wale watakaoruhusiwa kuketi katika ukumbi wa mijadala,” akawaambia wanahabari Alhamisi katika mkahawa wa Enashipai Spu, Naivasha.

Maseneta walikuwa wamekutana Naivasha kujadili ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI) iliyozinduliwa majuzi katika ukumbi wa Bomas, Nairobi.

Wakati huu, ni maseneta 30 kati ya 67 huruhusiwa kuingia kwenye ukumbi wa mjadlaa kwa wakati mmoja kama hatua ya kuzuia mtagusano miongoni mwao.

Ongezeko la idadi ya visa vya maambukizi ya virusi vya corona nchini haswa mwezi wa Oktoba umeibua hofu nchini huku serikali na wananchi wakilaumiwa kwa kulegeza uzingativu wa masharti ya kuzuia kuenea kwa virusi hivyo. Kwa mara ya kwanza tangu ugonjwa huo ulipozuka nchini, Kenya imeandikisha visa 1068 vya maambukizi ndani ya saa 24.

Idadi ya wagonjwa wanaofariki kutoka na Covid-19 pia imeongezeka kwa kiwango cha kuhofisha kiasi kwamba kuna siku ambapo jumla ya wagonjwa 16 walifariki kwa siku moja..

Hatima ya wanafunzi ambao hawajarejelea masomo haijulikana baada ya Wazari wa Elimu George Magoha kutangaza kuwa wizara yake ifanya mashauriano zaidi na wadau wengine “kufuatia ongezeko la visa vya maambukizi.”

Katibu katika Wizara hiyo Belio Kipsang’ Jumatano aliambia Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Elimu kwamba kufikia wakati huo visa vya maambukizi ya corona vimepatikana katika shule 35 kote nchini.

Alifichua kuwa jumla ya walimu 33, wanafunzi 17 na wafanyakazi wanane wa shule wamepatikana na virusi vya corona huku Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Tononoka, Mombasa, Mohammed Khamis akifariki kutokana na ugonjwa huo.

You can share this post!

Wanasoka 7 walioishia kuwa masupastaa baada ya kutemwa na...

BBI: Koma kuingilia IEBC, Ruto amwambia Raila