• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 5:55 AM
BBI: Koma kuingilia IEBC, Ruto amwambia Raila

BBI: Koma kuingilia IEBC, Ruto amwambia Raila

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto Ijumaa alimtaka kiongozi wa ODM Raila Odinga kukoma kukosoa makadirio ya gharama ya kura ya maamuzi ijayo yaliyotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Akiongea Ijumaa katika uwanja wa michezo ya Kago, eneobunge la Kangema, Kaunti ya Murang’a, Dkt Ruto alimtaka waziri huyo mkuu wa zamani kukoma kupinga makadirio ya IEBC kwamba shughuli hiyo itafyonza Sh14 bilioni.

“Achana na IEBC kwa sababu hata kura ya maamuzi iliyopita iligharimu Sh10 bilioni ilhali ni wapigakura milioni 12 pekee walishiriki. Sasa iweje kwamba watatumia Sh2 bilioni katika kura ya maamuzi itakayoshirikisha wapiga kura milioni 19?” Dkt Ruto akauliza.

“Hii haiwezi kufanyika! Kwa hivyo yule jamaa wa vitendawili akome kutudanganya. Yeye sio mtaalamu wa masuala ya uchaguzi; na wakome kudharau asasi hii ya kikatiba,” akaongeza.

Mnamo Alhamisi Bw Odinga alipuuzilia mbali makadirio yaliyowasilishwa na Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC Hussein Marjan, mbele ya wabunge kwamba kura ya maamuzi ya kufanikisha mageuzi ya katiba yaliyopendekezwa kwenye ripoti ya BBI, itagharimu Sh13.7 milioni.

Bw Marijan alisema hayo alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC) chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, kujibu maswali yaliyoibuliwa kwenye ripoti ya Mhasibu Mkuu wa Serikali kuhusu matumizi ya fedha katika tume hiyo katika mwaka wa kifedha wa 2017/2018.

Bw Marijan alisema gharama hiyo inayumuisha ile ya kuwaajiri maafisa wa kusimamia upigaji kura, maafisa wa usalama, uchapishaji wa karatasi za kura, miongoni mwa matumizi mengine.

“Tumekuwa tukijipanga kwa kura ya maamuzi na kufikia sasa tumekadirio kuwa itagharimu Sh13.7 bilioni. Hata hivyo, bado tunaendelea kufanya hesabu zetu,” akawaambia wabunge wanachama wa PAC.

Katika uchaguzi mkuu wa 2017, IEBC iliajiri jumla ya maafisa 350,000 wa kusimamia uchaguzi huo uliohusisha wapiga kura 19.7 milioni.

Lakini kwenye taarifa aliyotuma kwa vyombo vya habari jana, Bw Odinga alipuuzilia mbali makadirio hayo ya IEBC na kushikilia kuwa kura ya maamuzi ijayo itagharimu Sh2 bilioni.

“Haiwezekani kwa kura ya maamuzi kugharimu Sh14 bilioni. Hii  ni shughuli ambayo inaweza kugharimu Sh2 bilioni ikiendeshwa na watu wenye maadili na wasio na uchu wa kupora pesa za umma,” Bw Odinga akasema.

“Huu mwenendo wa IEBC kutumia pesa nyingi kiasi hiki ndio ndio mojawapo ya sababu inayopelekea msukumo wa kuifanyia mabadiliko na hata kuwaondoa makamishna wa sasa,” akaongeza.

Saa chache baadaye Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati naye alimrukia Bw Odinga akimtaja kama kutoa kauli za uwongo kuhusiana na suala nyeti kama hilo.

“Huyu Odinga anadanganya Wakenya kwamba kura ya maamuzi itagharimu Sh2 bilioni ilhali ile ya 2010 iligharimu Sh10.7 bilioni wakati ambapo yeye alikuwa serikali kama Waziri Mkuu,” akasema.

You can share this post!

Corona: Seneti kubadili taratibu za kuendesha shughuli

Mwalimu mkuu Tononoka aangamia kwa corona