• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
Fujo Tanzania upinzani ukipinga matokeo

Fujo Tanzania upinzani ukipinga matokeo

Na THE CITIZEN

GHASIA zilizuka na watu kadhaa wakakamatwa katika maeneo ambayo viongozi wa upinzani na wafuasi wao walikataa matokeo ya uchaguzi mkuu yaliyoanza kutangazwa Jumatano wakisema ulikumbwa na udanganyifu mwingi.

Hayo yalijiri huku Rais John Pombe Magufuli akiendelea kuongoza kwa idadi ya kura dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Tundu Lissu kufikia jana.

Kulikuwa na ripoti kwamba, polisi walikabiliana na vijana waliokuwa wakilalamikia matokeo katika ngome za upinzani kote nchini Tanzania.

Wagombeaji kadhaa wa upinzani na maajenti wao katika uchaguzi huo walikamatwa polisi walipokabiliana na waandamanaji waliokataa kukubali matokeo ya uchaguzi.

Ripoti kutoka Lindi zilisema, mali zikiwemo nyumba na magari katika maeneobunge ya Liwale, Nachingwea na Mtama yalichomwa au kuharibiwa vibaya Alhamisi wakazi walipoandamana kukataa matokeo kwenye vituo vya kupigia kura.

Nyumba ya mgombeaji wa Chama Chama Mapinduzi (CCM) eneobunge la Liwale, Zuberi Kuchauka, zahanati na ofisini za chama cha Civic United Front (CUF) pia zilichomwa wakati wa ghasia hizo.

Walioshuhudia pia waliambia gazeti la The Citizen kwamba, ambulensi moja pia ilichomwa.“Jana usiku, polisi waliimarisha usalama kuzuia hasara zaidi.

Tulisikia milio ya risasi na milipuko usiku wote,” alisema mkazi mmoja.Alisema watu kadhaa walikamatwa na wengine walijeruhiwa maafisa wa usalama walipokuwa wakizima ghasia hizo.

Katika mji wa Nachingwea, gari la polisi lilichomwa na wakazi wa kijiji cha Mpiluka waliokuwa na hasira wakipinga matokeo yaliyotangazwa kituoni kuonyesha wagombeaji wa CCM walishinda.

“Katika eneo hili, vijana wengi wanaunga upinzani na kwa hivyo walizua ghasia kuonyesha kutoridhishwa kwao na matokeo,” mkazi mmoja aliambia ‘The Citizen’ kwa simu.

Ripoti kutoka eneobunge la Mtama zilisema watu waliokuwa na ghadhabu walichoma afisi ya mkuu wa wadi mnamo Jumatano.

“Ujumuishaji wa kura uliokuwa ukiendelea eneo hilo ulilazimika kuhamishiwa Nyangao kufuatia hofu ya usalama,” alisema mkazi aliyeshuhudia.

Mgombea kiti cha ubunge wa CCM, Zuberi Kuchauka alisema ghasia zilianzia kituo cha kupigia kura cha Likongowele ambapo wagombeaji wa upinzani walitaka wapewe nakala za matokeo jambo ambalo alisema sio lazima kufuatia mabadiliko yaliyofanyiwa sheria ya uchaguzi.

Msimamizi wa uchaguzi wilayani Mpwapwa Sweya Mamba alithibitisha visa hivyo lakini akasema havikuathiri matokeo ya uchaguzi. Fujo ziliripotiwa Shinyanga ambapo polisi walimkamata mgombeaji wa kiti cha ubunge wa chama cha Chadema Salome Makamba.

You can share this post!

BBI: Matiang’i aonya polisi dhidi ya kutumiwa na...

Hofu corona ikizidi kusambaa shuleni, serikali ikisisitiza...