• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
KRA yasema itaendelea kukusanya ushuru licha ya Bunge kufuta sheria 23

KRA yasema itaendelea kukusanya ushuru licha ya Bunge kufuta sheria 23

Na CHARLES WASONGA

MAMLAKA ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) imefafanua kuwa itaendelea kukusanya ushuru kwa kutumia sheria zilizopitishwa na Bunge la Kitaifa pasi na na kushirikishwa kwa Seneti.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Ijumaa, Oktoba 30, 2020, KRA ilisema kuwa ina muda wa miezi sita kuendelea kutumia sheria hizo, kipindi ambacho kilitolewa na mahakama kwa bunge la kitaifa kuhakikisha kuwa limetoa nafasi kwa mchango wa Seneti.

Mnamo Alhamisi majaji watatu wa mahakama kuu walibatilisha sheria 23 zilizopitishwa na bunge la kitaifa mnamo 2018, ikiwemo Sheria ya Fedha ya 2018, bila mchango wa Seneti hatua ambayo walisema ni kinyume cha Katiba.

“Licha ya kubatilishwa kwa sheria hizo, utekelezaji wa amri ya mahakama ulisimamishwa kwa miezi tisa ili kumtoa nafasi wa Spika wa Bunge la Kitaifa na Mkuu wa Sheria kutimiza matakwa ya kipengele cha 110 ibara ya 3 ya Katiba na kuhalalisha sheria hizo,” akasema Paul Mutuku ambaye ni Kamishna wa KRA anayesimamia kitengo cha Huduma za Kisheria na Ushirikishi wa shughuli za Bodi.

Katika uamuzi wao Majaji Jairus Ngaah, Anthony Ndung’u na Teresia Matheka walisema kwa kutohusisha Seneti katika upitishwaji wa sheria hizo, Bunge la Kitaifa lilikiuka kipengele hicho cha Katiba kinachasema kwamba “Maspika wa Bunge la Kitaifa na Seneti wanatatua suala kuhusu iwapo Mswada unahusu kaunti au la na kama ni mswada spesheli au ni kwa kawaida.”

Ijumaa Bw Mutuku aliongeza kufuata hatua ya mahakama hao kusimamisha utekelezaji wa uamuzi wao kwa miezi tisa, hadi Julai 2021, utekelezaji wa sheria husika na KRA “ungali halali.”

Sheria zingine zinazoathiri KRA zilizobatilishwa kando na Sheria ya Fedha ya 2018 ni; Sheria za Marekebisho ya Sheria za Ushuru ya 2018 (Tax Amendment Laws, 2018) na Sheria ya Mabadiliko ya Sheria mbalimbali za Serikali, ya 2018 (Staute Law Miscellaneous Amendment, 2018).

Sheria ya Fedha ya 2018 ndio ilipelekea kampuni ya kamari ya Sportpesa kugura Kenya kwa kushindwa kumudu hitaji la kulipa ushuru wa asilimia 20 kutokana na fedha zote ambazo wacheza kamari watashinda. Hii ni kando na ushuru wa asilimia 25 ya faida ambao serikali hutoza kampuni zinazoendesha shughuli zao humu nchini.

Ushuru mwingine ulianzishwa chini ya sheria hii ni ule thamani ya ziada (VAT) ya asilimia 8 kwa bei ya petroli na dizeli ambayo ilianza kutumika mnamo Septemba 2018. Kuanzishwa kwa ushuru huu kulichangia kupanda kwa bei ya bidhaa hizi na hivyo kuwakera watumiaji kwa kupandisha gharama ya maisha.

Mipango ya kuanzishwa kwa ushuru wa VAT kwa mafuta ilikuwa imeahirishwa tangu 2013.

Sheria hiyo pia iliongeza ushuru unaotozwa huduma za kupokea na kutumia pesa kwa njia ya simu kama vile M-Pesa na huduma nyinginezo husika.

Awali, kampuni ya Safaricom ilikuwa imepinga nyongeza ya ushuru kwa ada zinazozwa huduma za kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu ikisema hatua hiyo itawaumiza watu wengi masikini, wengi wasio na akaunti za benki na hutegemea huduma za M-Pesa.

Familia zenye mapato ya chini ziliathirika zaidi na kupitia sheria hiyo ya Fedha ya 2018 kwani ilianzisha ada ya Sh18 kwa lita kwa mafuta taa. Hatua hii ililenga kuzima mienendo ya baadhi ya kampuni na watu binafsi kuchanganya mafuta taa na petroli au dizeli kisha kuwauzia wanunuzi wasio na ufahamu kuhusu uovu huo.

Mamlaka ya kusimamia sekta ya kawi inasema kuwa kufuatua kuanzishwa kwa ada hiyo matumizi ya mafuta taa ilipungua mwaka jana hadi lita 15 milioni kutoka lita 40 milioni hapo awali.

Marekebisho ya sheria ya ushuru ya 2018 yaliyoanzisha hitaji kwamba wafanyabiashara wadogo kama mama mboga na wasusi kulipa ushuru wa kima asimilia 15 ya ada ya leseni za biashara ambazo hutolewa na serikali za kaunti pia imeathirika na uamuzi wa majaji hao watatu.

Ushuru huo unaojulikana kwa kimombo kama “presumptive tax” ulitoa nafasi kwa KRA kukusanya data zaidi kuhusu wafanyabiashara wadogo na hivyo kutoa nafasi kwa kuanzishwa kwa ushuru unaotozwa faida za wafanyabiashara hao, almaarufu, “turnover tax”

Sheria nyingine iliyoathirika na uamuzi huo wa Mahakama Kuu ni Sheria ya Marekebisho ya sheria za kitaifa za Afya ya 2018.

Sheria hiyo iliipa Mamlaka ya Usambazaji Dawa na Vifaa vya Kimatibabu (Kemsa) ukiritimba wa kuziuzia serikali za kaunti dawa na vifaa vinginevyo vya kimatibabu. Serikali hizo zimekuwa zikilalamikia sheria hiyo zikisema zimezuiwa kununua dawa kutoka kwa kampuni zingine ilhali Kemsa huwauzia dawa kwa bei ghali mno.

Sheria nyingine iliyobatilishwa na ile inayodhibiti uhalifu unaendeshwa kupitia mitandao na kompyuta (Computer Cyber Crime Act) ambayo imekuwa ikitumia kuwadhibiti wanablogu na watumizi wengine wa mitandao dhidi ya kueneza chuki, vitisho na jumbe zingine chafu.

Sheria iliyochangia kuanzisha kwa mpango wa usajili wa wananchi kidijitali mwaka jana ili wapewe Huduma Namba pia inakabiliwa na hatari ya kubatilisha ikiwa Bunge la Kitaifa haliipeleka kwa Seneti kwa idhini yake.

You can share this post!

BBI: Wafuasi wa Ruto wasema mkutano wa Naivasha haufai

Naibu Gavana akejeli wanasiasa wanaolipa vijana kuvuruga...