• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Ukaidi wa Ruto unavyoweza kumjenga au kumbomoa kisiasa 2022

Ukaidi wa Ruto unavyoweza kumjenga au kumbomoa kisiasa 2022

Na BENSON MATHEKA

Amelaumiwa kwa kumdharau na kumkaidi Rais Uhuru Kenyatta kufuatia msimamo wake kuhusu handisheki na mchakato wa kubadilisha katiba.

Ingawa Naibu Rais William Ruto amekuwa akieleza msimamo wake kwenye mikutano mbalimbali, hakuwa amepinga mpango huo hadharani mbele ya rais hadi Jumatatu katika ukumbi wa Bomas aliposema kwamba mapendekezo ya ripoti ya Jopokazi la Maridhiano ( BBI) sio suluhu kwa matatizo ya Wakenya.

Alikuwa kiongozi wa pekee katika kongamano la kuzindua ripoti hiyo aliyeikosoa bila kupesa mboni za macho yake na kufanya wajumbe waliohudhuria kumzomea.Dkt Ruto alisema hajashawishika kuwa mapendekezo yaliyo katika ripoti hiyo yatatimiza malengo ya kuunganisha Wakenya.

Akizingumza mbele ya Rais Uhuru Kenyatta na mshirika wake katika mchakato huo Raila Odinga, Dkt Ruto alikosoa mapendekezo ya kubadilisha Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC), pendekezo la kubuni wadhifa wa afisa wa kupokea malalamishi katika mahakama atakayeteuliwa na rais na hatua za kupokonya seneti jukumu la kuamua mgao kwa kaunti.

Vilevile, alikosoa pendekezo la kubuniwa kwa baraza la polisi litakalosimamiwa na waziri wa usalama wa ndani na hatua ya kubuni nyadhifa za waziri mkuu na manaibu wake.

Alionya dhidi ya kuunga baadhi ya mapendekezo akisema yanaweza kutumiwa kuwadhulumu wale wanaoyashinikiza.Dkt Ruto alitaja hatua ya kubuni wadhifa wa afisa wa kupokea malalamishi kuhusu mahakama kama itakayopokonya idara hiyo uhuru wake na kuifanya ithibitiwe na serikali kuu.

Alisema mahakama inafaa kutengewa pesa zaidi kujenga korti nchini ili kuimarisha utoaji wa haki kwa Wakenya. Kulingana na wadadisi wa kisiasa, msimamo wa Dkt Ruto huenda ukazidisha uhusiano wake baridi na Rais Kenyatta au kuuimarisha.

“Kuna wanaodai kwamba anamkaidi Rais na kwamba alionyesha kiburi chake mbele ya kiongozi wa nchi katika kongamano muhimu lakini ukweli wa mambo ni kuwa katika mchakato muhimu kama kubadilisha katiba, maoni ya kila mmoja ni muhimu,” asema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

Anasema kwamba ingawa Rais alisema kwamba alimshirikisha Dkt Ruto katika kila hatua ya mchakato huo, hiyo haimaanishi kwamba anafaa kukubali mapendekezo yasiyomridhisha.

Mchanganuzi wa siasa Mutahi Ngunyi anahisi kuwa Dkt Ruto alikosea kwa kuanika kiburi chake mbele ya kiongozi wa nchi. “Wengi wanakubaliana kuwa William Ruto alijianika katika Bomas. Kufikia sasa anafaa kuelewa kwamba kila wakati mtu hafai kuwa sahihi, narudia kusema kuwa yeye amekuwa kipofu katika chumba chenye giza akifuata paka mweusi ambaye hayumo,” asema Ngunyi.

Washirika wa kisiasa wa Dkt Ruto wanahisi kwamba ana haki ya kidemokrasia ya kujieleza na kutofautiana na viongozi wengine kuhusu masuala ya kitaifa.

“Hakuna makosa kueleza msimamo wako kuhusu masuala yenye umuhimu wa kitaifa kama kubadilisha katiba. Huo sio ukaidi, sio kiburi, ni haki iliyohakikishiwa kila mmoja na katiba ya Kenya na haifai kunyimwa mtu yeyote,” asema mbunge wa Soy Caleb Kositany.

Mbunge huyo alisema maoni ya Dkt Ruto ni ya Wakenya wengi wanaohangaika kupata riziki. Dkt Ruto aliambia wajumbe waliokuwa wakimzomea alipokuwa akiwahutubia Bomas kwamba anawakilisha mamilioni ya mahasla nchini.

Kulingana na Kamwanah, wanaodai kuwa Dkt Ruto ana kiburi ni wale wanaotumika kama vibaraka wa wengine. “Kwa kukataa kuwa kibaraka wa kuidhinisha BBI ambayo amesema sio mbaya lakini maoni ya kila mtu yanafaa kushirikishwa, Dkt Ruto amekataa kuwa kibaraka. Kuwa na msimamo na kuushikilia sio hatia baadhi ya watu wanavyodai,” asema.

Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen anasema Dkt Ruto alionyesha ujasiri wa kipekee kwa kufichua mapengo na udhaifu wa ripoti ya BBI.

Aliwaambia waliomzomea Dkt Ruto katika kongamano la Bomas kwamba mchakato wa kubadilisha katiba hauhitaji hasira. “Waliomzomea Dkt Ruto huko Bomas walijipatia aibu ndogo ndogo. Mliambiwa hii kitu inataka mdahalo na kama huna cha kusema usilete makasiriko,” Bw Murkomen alisema.

Alisema waliozungumza katika kongamano hilo walikuwa wamefunzwa ya kusema isipokuwa Dkt Ruto. Wadadisi wanasema ingawa Dkt Ruto na Rais Kenyatta wametofautiana kimaoni kuna wanaochukulia kuwa naibu rais ana kiburi na ni mkaidi.

Hii ndiyo imefanya atengwe serikalini hatua ambayo imefanya umaarufu wake kuongezeka mashinani miongoni mwa Wakenya masikini ambao amejitambulisha nao.

“Kwa kumchukulia kuwa mwenye kiburi na mkaidi, wanaompiga vita wataendeleza kampeni dhidi yake kwamba anavuruga ajenda muhimu kama BBI. Sidhani huu ni ukweli na kwa kufanya hivi, umaarufu wake unaweza kuongezeka,” asema mdadisi wa siasa Joseph Katana.

Anasema kauli za baadhi ya washirika wa rais kwamba hakuna maoni mapya yatakayokubaliwa kurekebisha ripoti ya BBI, zinaonyesha kwamba Dkt Ruto anasema ukweli kwamba mchakato huo unalenga kunufaisha watu wachache na kukadamiza masikini.

Mnamo Alhamisi, Naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe alipuuza wanaotoa mapendekezo mapya kuhusu ripoti hiyo akisema haitarekebishwa.

Kulingana na Bw Murathe, wanaoikosoa wanataka kucheleweshwa mchakato huo. Hii ni licha ya Rais Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ambao ndio waasisi wa BBI kusisitza kuwa maoni yanakaribishwa.

“Kauli za akina Murathe zinaweza kumjenga Dkt Ruto mashinani watu wakiamini kuna njama fiche BBI. Kampeni ya kumsawiri kama kichwa ngumu imekosa kufaulu hata kwa kutumia polisi kuzima mikutano yake. Amejitokeza kama kiongozi mwenye mawazo huru, jasiri, mkakamavu na mwenye msimamo. Hii haifurahishi wanaohisi amekuwa tisho kwa mipango yao,” asema Katana.

You can share this post!

BBI: Mtihani kwa Matiang’i ‘Reggae’...

Kibarua cha Joho na Kingi kuuza BBI eneo la Pwani