• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 9:50 AM
Kibarua cha Joho na Kingi kuuza BBI eneo la Pwani

Kibarua cha Joho na Kingi kuuza BBI eneo la Pwani

?Na MOHAMED AHMED

NGOMA ya ripoti ya Jopokazi la Mpango wa Maridhiano (BBI) ikiendelea kurindima, ni dhahiri kuwa viongozi wengi wameoenekana kuiunga mkono ripoti hiyo.

Licha ya viongozi hao wengi kuipigia debe BBI, imedhihirika kuwa mengi ambayo yalikuwa yamependekezwa kutoka maeneo tofauti ya viongozi hao hayakuzingatiwa katika ripoti hiyo.

Miongoni mwa maeneo hayo ni kanda ya Pwani ambayo licha ya viongozi wake kutoa mapendekezo 16 wakitaka yazingatiwe na BBI, imeibuka kuwa hakuna lolote lile ambalo linagusia maendeleo ya Wapwani ambalo limehusishwa kwenye ripoti hiyo.

Wakiongozwa na magavana wa Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi Amason Kingi ambao wametajwa kuwa ndio ambao wataongoza gurudumu la kuiuza BBI kwa wakazi wa Pwani, wachanganuzi wa siasa sasa wanasema kuwa huenda wawili hao wakawa na wakati mgumu iwapo kutaibuka makundi yatakayowauliza maswali kuhusiana na masuala yaliopendekezwa kutoka Pwani.

Miongoni mwa mambo muhimu ambayo Bw Joho na Bw Kingi walikuwa wamewasilisha kwa niaba ya wakazi wa Pwani mnamo mwezi Januari ni pamoja na kutelekezwa kwa ripoti ya dhulma za kihistoria za ardhi za TJRC na ile ya Ndung’u.

Magavana hao vilevile walipendekeza kuwa operesheni za uchukuzi ziendelezwe kwenye bandari ya Mombasa. Ili kuwezesha ukuzaji wa uchumi viwanda vya nazi, korosho, sim sim na pamba miongoni mwa mimea mengine kutoka Pwani.

Aidha, walipendekeza kuwepo kwa wizara ya masuala ya bahari ambayo itasimamiwa na waziri kutoka eneo la Pwani.Bw Joho na Bw Kingi pia walipendekeza kuwa Pwani igawanywe sehemu mbili ambazo zitatambulika kuwa Pwani ya Chini (Mombasa, Kwale na Taita Taveta) na Pwani ya Juu (Kilifi, Lamu na Tana River).

Pendekezo hilo lilitafsiriwa kama njama ya wawili hao kutaka kusalia mamlakani hata baada ya kumaliza hatamu zao za uongozi kama magavana.Hata hivyo, yote hayo yakiwemo masuala ya nafasi za kisiasa, dhuluma za ardhi na ukuzaji uchumi, yameonekana kupuuziliwa mbali katika ripoti hiyo ya BBi.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa za Pwani Profesa Hassan Mwakimako, suala la BBI limeibuka kuangazia zaidi mambo ambayo yanahusiana na viongozi wawili ambao wanaendesha hoja hiyo ambao ni Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“Hata katika ripoti hiyo, ni wazi kuwa hakuna masuala ambayo yanahusu mwananchi ya kawaida ambayo yamezingatiwa kikamilifu na sio yale ya Pwani pekee bali ya nchi nzima kwa jumla. Ni wazi kuwa hii ni ripoti ambayo itawafaa wachache pekee,” akasema Prof Mwakimako.

Alisema kuwa Bw Joho na Bw Kingi huenda wakawa na wakati mgumu kuuza sera za BBI kwani imejitokeza wazi kuwa haijihusishi na maslahi ya Wapwani.

Aidha, Prof Mwakimako aliongeza kuwa kutohusishwa kwa mapendekezo ya wawili hao katika ripoti hiyo kumewaonyesha wazi kuwa wao ni kama hawatambuliwi katika hoja zao.Licha ya mapendekezo mengi ya watu wa Pwani kutozingatiwa katika ripoti hiyo, Bw Kingi na Bw Joho tayari wameunga mkono ripoti hiyo ambayo wameanza kuipigia debe kwa kishindo.

Wakati wa siku kuu ya Mashujaa wawili hao walijitosa kimasomaso na kutoa wito kwa wakazi kuwataka waunge mkono BBI.

Huku mchakato wa BBI ukianza kushika kasi ili kuhakikisha kuwa nchi inaenda katika kura ya maoni na kubadilisha katiba, itasubiriwa kuonekana vile mambo yatakavyokwenda huku ikijitokeza wazi kuwa baadhi ya wabunge wa Pwani ni miongoni mwa wale ambao wanapinga ripoti hiyo.

You can share this post!

Ukaidi wa Ruto unavyoweza kumjenga au kumbomoa kisiasa 2022

Je, Sonko anajichongea kumshambulia Rais?