Infotrak yakanusha madai ya gavana kuhusu hongo
Na IBRAHIM ORUKO
KAMPUNI ya Infotrak imekanusha madai ya Gavana wa Meru, Kiraitu Murungi kwamba, wahudumu wake waliitisha hongo kutoka kwa baadhi ya magavana ili kuwaorodhesha vyema katika ripoti yake ya hivi majuzi kuhusu utendakazi wa kaunti.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bi Angela Ambitho, alimtaka Bw Murungi kuandikisha taarifa kwa mashirika yanayohusika na uchunguzi kuhusu madai hayo ya ufisadi.
“Ninawataka waende na kuripoti uhalifu huo kwa polisi na kueleza ni lini kitendo hicho kilifanyika, ni nani aliyehusika na katika mazingira yapi,” Bi Ambitho alieleza Taifa Leo.
Kulingana naye, ada pekee iliyokuwa ikitozwa na shirika hilo ilikuwa Sh3 milioni za kugharamia data iliyokusanywa katika maeneo husika wakati wa utafiti.
Alisema kuwasilisha data hiyo kwa magavana hakukutozwa ada yoyote lakini gharama ya kukusanya data ilitwikwa viongozi wa kaunti waliotaka kukabidhiwa ripoti kamili ya matokeo ya utafiti huo.
Alisema kiasi hicho cha Sh3 milioni kiligharimia usafirishaji wa watafiti kutoka pembe moja ya kaunti hadi nyingine na kuandaa ripoti kamilifu, ambayo alisema haingetolewa bila malipo.
“Shughuli hii huwa na ada, sawa na ada ya huduma za kisheria. Haimaanishi kuwa nafasi yako kwenye orodha itabadilika. Ikiwa ulishikilia mkia katika sekta fulani itasalia vivyo hivyo,” alisema.
Orodha ya kufuatilia utendakazi wa magavana iliorodhesha uwezo wa kila mmoja katika vitengo vyote vya ugatuzi; afya, kilimo, elimu, barabara, kawi, huduma za jamii, elimu ya watoto wachanga, utalii, biashara, makazi na utoaji makao miongoni mwa mengine.
Katika ripoti hiyo, Bw Murungi, aliyewahi kuwa waziri, aliorodheshwa miongoni mwa magavana wenye utendakazi duni katika eneo la mashariki.