• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
DPP kuwasilisha mashahidi 30 kwa kesi ya Jumwa

DPP kuwasilisha mashahidi 30 kwa kesi ya Jumwa

Na BRIAN OCHARO

MASHAHIDI 30 wanatarajiwa kutoa ushahidi wao katika kesi ya mauaji inayomkumba Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa na msaidizi wake, Geoffrey Otieno Okuto.

Naibu Mkurugenzi wa kuongoza mashtaka katika Kaunti ya Mombasa, Bw Alloys Kemo alisema Jumanne kuwa, tayari mashahidi hao wameorodheshwa.

“Ushahidi mwingine utafikishwa mahakamani baadaye leo,” akasema Kiongozi huyo wa mashtaka.

Bi Jumwa na Bw Okuto walifika mbele ya Jaji Anne Ong’injo katika mahakama kuu, Jumanne.

Jaji huyo ametenga siku tatu mfululizo ambazo kesi hiyo itasikilizwa, na mashahidi wanne watasimama kizimbani kwa kila siku.

Kesi hiyo itaanza kusikilizwa mnamo Februari 2, 3 na 4 mwaka ujao.

Pia, mahakama hiyo iliagiza mashahidi hao waorodheshwe na washukiwa wapewe nakala zao kabla ya siku ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa.

Wakili wa washukiwa hao, Jared Magolo alithibitisha kuwa tayari washapata karatasi za korti zenye taarifa zilizoandikishwa na mashahidi hao.

“Tuko tayari kesi hiyo ianze kusikilizwa,” akasema Bw Magolo.

Bi Jumwa na mshukiwa mwenzake walikuwa wameiomba mahakama iwapunguzie dhamana, lakini baadaye waliiondoa.

Washukiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya mfuasi mmoja wa chama cha ODM, Bw Joja Ngumbau ambayo yalitokea mnamo Oktoba 15, 2019, wakati wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa wadi ya Ganda.

Wawili hao walikanusha mashtaka hayo walipofika mahakamani Oktoba.

You can share this post!

Kipruto na Cherono waahidi makuu katika Valencia Marathon

Wito serikali iongeze maabara za nyama