Kimataifa

Maandamano Amerika Trump akipinga matokeo ya kura

November 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

WASHINGTON D.C., Amerika

MAANDAMANO Alhamisi yalitanda katika maeneo mbalimbali ya Amerika, baada ya Rais Donald Trump kupinga matokeo.

Trump aliwasilisha malalamishi mahakamani kupinga matokeo ya kura za urais katika baadhi ya majimbo ambapo mpinzani wake wa karibu, Joe Biden alishinda.

Maafisa wa usalama walikabiliana na waandamanaji, baadhi wakiunga mkono kauli ya Rais Trump na wengine wakimkashifu huku uharibifu ukishuhudiwa baadhi ya maeneo.

Katika maeneo ya Minneapolis na Portland, baadhi ya waandamanaji walinyakwa na maafisa wa polisi walipokuwa wakizuia ghasia.

Mamia walikuwa wamekusanyika kupinga kura kuhesabiwa upya huku wakivunja madirisha ya maduka na kukabiliana na maafisa wa polisi.

Katika mji wa Phoenix, zaidi ya wafuasi 150 wa Rais Trump walikusanyika nje ya afisi ya tume ya uchaguzi ambapo walifuatilia kwa karibu shughuli za kuhesabu kura, baadhi wakiwa na silaha.

Waandamanaji katika maeneo mbalimbali ya Phoenix walidai afisa wa uchaguzi Adrian Fontes ambaye alikuwa akisimamia uchaguzi kwenye Kaunti ya Maricopa, hakuwa akihesabu kura za Rais Trump kwenye kaunti hiyo ambayo ina wapigakura wengi katika Jimbo la Arizona.

Hata hivyo, hakukuwa na ushahidi wowote kuwa udanganyifu ulikwepo kwenye jimbo hilo muhimu kwa Rais Trump na Biden.

Mjini Detroit, kundi la waandamanaji wanaounga mkono Rais Trump walikusanyika nje ya kituo cha kuhesabu kura wakitaka shughuli hiyo isitishwe mara moja. Hii ni baada ya kikosi cha kampeni cha Rais Trump kuwasilisha kesi ya kusimamisha shughuli hiyo katika jimbo la Michigan.

Waandamanaji pia walikusanyika katika miji ya Philadelphia, Los Angeles, Chicago na mengine huku maandamano zaidi yakitarajiwa siku zijazo.

Jijini Minneapolis, mamia ya waandamanaji walikabiliana na polisi walipoonyesha wazi ghadhabu zao kuhusu matamshi ya Rais Trump.

“Hatutamruhusu Donald Trump kuiba uchaguzi huu licha ya raia wa Marekani kumchagua Joe Biden,” akasema wakili Nekima Levy ambaye alikuwa kati ya waandamanaji hao.

Polisi ambao baadhi walikuwa wamebebwa na farasi waliwakamata baadhi ya waandamanaji na kuwatawanya wengine.

Jijini New York maandamano ya amani yalishuhudiwa, huku wakitoa wito kuwe na uwazi kwenye hesabu za kura na pia kukemea tofauti za ubaguzi wa rangi ambazo zimeanza kuchipuka baada ya kura ya Jumanne.

Hata hivyo, hali ilibadilika baadaye na ghasia kuzuka, maafisa wa polisi wakiwakamata waandamanaji zaidi ya 20.

Kule Portland, mamia waliandamana wakitembea jijini wakisema uchaguzi umeisha na raia wa Marekani wanafaa waruhusiwe waendelea na maisha yao kama zamani.