• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Taharuki Lamu baada ya mzee na mwanawe kuuawa kinyama

Taharuki Lamu baada ya mzee na mwanawe kuuawa kinyama

Na KALUME KAZUNGU

TAHARUKI imetanda kijijini Mulei, tarafa ya Mpeketoni, Kaunti ya Lamu baada ya kijana wa  umri wa miaka 22 kuwakatakata kwa upanga na kuwaua mzee aliyekuwa na umri wa miaka 75 na mtoto wake aliyekuwa na umri wa miaka 23 Ijumaa.

Kulingana na majirani, mshukiwa alifika ghafla kwenye boma la Mzee Gojama Wario akiwa amejihami kwa upanga.

Baada ya kumuuliza maswali mzee huyo, mshukiwa alimrukia na kumkatakata kwa upanga kichwani na miguuni na kumuua.

Baadaye alimvamia mtoto wa mzee huyo kwa jina, Yusuf Gojama Wario ambapo alimkata kwa upanga tumboni na kumuua papo hapo kabla ya kutorokea msituni.

Mmoja wa majirani Salim Godana alisema mshukiwa alikuwa amewasili kijijini hivi majuzi baada ya kutoweka kwa zaidi ya miezi mitatu.

“Ni kijana ambaye hakai sana hapa kijijini kwetu. Aliingia tu wiki chache zilizopita. Huwa anaishi peke yake kwani hana familia hapa. Tumeshangazwa na kitendo chake cha kumuua mzee na mwanawe hapa Mulei. Ni jambo ambalo limetutia hofu,” akasema Bw Godana.

Bi Mary Kariuki alisema mzee aliyeuawa alikuwa mwenyekiti wa kamati ya amani kijijini Mulei na akataja kifo chake kuwa pigo kubwa kwa jamii ya eneo hilo.

Aliiomba idara ya usalama kuchunguza kwa makini tukio hilo na kuhakikisha mhusika wa mauaji hayo anakamatwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

“Familia yam zee Gojama haijakuwa na kisasi na mtu yeyote. Mzee ni mtu anayependa amani nah ii ndiyo sababu ni mmoja wa wanakijiji waliojitolea kuhubiri amani eneo hili. Tumeshangazwa na kitendo cha mshukiwa cha kumuua mzee na mwanawe ambao hawana hatia,” akasema Bi Kariuki.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia amethibitisha tukio hilo na kusema kuwa mshukiwa tayari amekamatwa na anazuiliwa kwenye kituo cha polisi mjini Mpeketoni.

Aliwataka wakazi kukoma kujichukulia sheria mikononi mwao kila wakati tofauti zinapozuka miongoni mwao.

“Ni masikitiko kwamba mshukiwa amewavamia na kuwaua baba na mwanawe eneo la Mulei. Polisi tayari wamemkamata na tutamfikisha kortini wakati wowote. Pia lazima mshukiwa achunguzwe akili kama iko sawa. Tukio alilofanya si la kawaida,” akasema Bw Macharia.

Miili ya waliouawa imepelekwa kwenye hifadhi ya maiti ya hospitali ya Mpeketoni.

Si mara ya kwanza kwa watu kuvamiana, kukatana, kujeruhiuana na hata kuuana kwa mapanga Lamu.

Mnamo Juni 2020, msichana wa umri wa miaka 14 ambaye ni mwanafunzi wa Darasa la Nane alijeruhiwa vibaya kwa upanga kichwani, miguuni na mikononi na babake mzazi aliyempata akisemezana na wanaume kwenye mtaa mmoja wa mji wa Hindi.

Julai 2020, mwanamume Yusuf Mohamed, ambaye alikuwa akifanya kazi ya kipato cha kutosheleza tu mahitaji ya siku, alivamiwa na kuuawa kwa kukatwa kwa mapanga na watu wasiojulikana eneo la Kizingitini.

Mnamo Septemba, 2018, mwanamume Issa Hussein Shidho, aliuawa kwa kuchomwa kisu tumboni mara kadhaa na mzee wa umri wa miaka 68 wakati huo baada ya ugomvi uliohusu miraa kuzuka baina yao eneo la Kiangwe, Lamu Mashariki.

You can share this post!

UMBEA: Mwanamke unapaswa kuvaa uhusika wa kike, sio jike...

Mwanahabari ni miongoni mwa waliouawa kwenye ghasia Kabul