Wakulima wa kahawa Kiambu wataka uboreshaji wa kilimo cha zao hilo
Na LAWRENCE ONGARO
WAKULIMA wa kahawa wa Kiambu, wapatao 100 walikongamana mjini Thika ili kuhamasishwa kuhusu kilimo bora cha zao hilo.
Wengi wao walitoa malalamiko yao jinsi ambavyo wamekuwa wakinyanyaswa na mawakala, wanapopeleka kahawa yao kwa kiwanda cha usagaji.
Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alikuwa mstari wa mbele kuwahamasisha na kuwapa mwelekeo wa jinsi wanavyostahili kuendesha kilimo chao cha kahawa.
Hata ingawa wengi wao hukuza hata zao la macadamia na majanichai bado wakulima hao walielezwa umuhimu wa kustawisha kilimo cha kahawa.
Bw Wainaina alisema tangu usimamizi mpya wa sekta ya kahawa (New KPCU) kuzinduliwa, wakulima wengi wameanza kuona faida ya kupeleka kahawa yao huko.
Alisema usimamizi mpya umeleta mwamko mpya na sasa wakulima wengi wana matumaini ya kunufaika kutokana na zao hilo.
“Ili muweze kufaidika vilivyo itakuwa vyema kujiunga kwa vikundi vya wakulima 10 au zaidi ili matakwa yenu yaweze kutatuliwa kikamilifu,” alisema Bw Wainaina.
Hata hivyo aliwataka wawe na kahawa safi ili waweze kunufaika pakubwa.
Alimpongeza Waziri wa Kilimo Bw Peter Munya ambaye alimtaja kama kiongozi anayebadilisha sekta ya kilimo na kuwa ya kutamanika na wakulima wengi.
Aliwashauri wajipange na kampuni ya kifedha ya kutoa mikopo aina ya J-Hela ambayo lengo lake kuu ni kuinua maisha ya wakulima.
“Iwapo utajiunga na kampuni hiyo ya J- Hela utaruhusiwa kukopa na kupokea mara tatu ya fedha zile uko nazo kwenye hazina yako,” alisema Bw Wainaina.
Bi Joyce Njeri ambaye ni mkulima wa Kahawa eneo la Gatundu Kaskazini alisema yeye kama mkulima hajanufaika pakubwa na zao hilo jinsi alivyotarajia.
Naye Lawrence Mwangi ambaye pia ni mkulima wa kahawa akielezea masaibu anayopitia, “Nimekuwa mkulima wa kahawa kwa muda mrefu lakini bado sijapata faida ya jasho langu kamili.”
Naye mbunge huyo alisema yeye kama mmoja kati ya wabunge kwenye kamati ya mauzo bungeni, atafanya juhudi kuona ya kwamba haki ya mkulima inalindwa vilivyo.
“Sitaki kuona wakulima hasa wa kutoka mashinani wakitaambika na zao la kahawa. Kwa hivyo nitawatetea vilivyo hadi mwisho,” alisema Bw Wainaina.
Aliiomba serikali kuwaadhibu vikali wanaokiuka sheria na kanuni za kilimo hasa kahawa.
“Tunataka kuona wakulima wakirudia ile hadhi ya kitambo ya kupata faida katika zao hilo. Hatutaki kuona mkulima akisononeka tena. Tunataka kila mkulima ajitokeze na kusema kuwa zao hilo la kahawa limemsadia kwa njia moja ama nyingine,” alifafanua.