Mamlaka kuharibu bidhaa ghushi za thamani ya Sh100 milioni
Na WACHIRA MWANGI
MAMLAKA ya Kudhibiti Bidhaa Ghushi (ACA), inatarajiwa kuteketeza bidhaa haramu zenye thamani ya Sh100 milioni Jumatatu.
Kaimu mwenyekiti wa ACA, Bi Fridah Kaberia alisema kubaribiwa kwa bidhaa hizo ni onyo kwa wafanyabiashara ambao wamebobea kuingiza bidhaa haramu nchini kisha kuwapunja wanunuzi.
“Hili ni onyo kwamba hatutakubali bidhaa haramu kuingizwa nchini. Tutaendelea kupambana na wanaoshiriki biashara hiyo hadi wakome kabisa,” akasema Bw Kaberia.
Akizungumza kwenye kikao na wanahabari mjini Mombasa, Bi Kaberia alisema uingizaji wa bidhaa haramu nchini huwapa hasara wafanyabiashara wanaouza bidhaa halali.Kulingana na utafiti uliofanywa mnamo 2018 na ACA, uingizaji wa bidhaa haramu ulisababishia nchi hasara ya Sh153.1 bilioni baada ya wanaohusika kunufaika kwa kupata Sh862 bilioni.
Kila mwaka, Kenya hupoteza Sh100 bilioni kwenye biashara hiyo haramu huku watengenezaji bidhaa wakikadiria hasara ya Sh68.75 bilioni huku nafasi 9,158 za ajira zikipotea.
Kulingana na ripoti hiyo, nafasi za uwekezaji ambazo ni za thamani ya Sh36.16 bilioni pia zilipotea kutokana na juhudi kali za kupambana na mauzo ya bidhaa haramu.Hata hivyo, alisema vita dhidi ya bidhaa ghushi vimekuwa vikikosa kufanikiwa kwa kuwa umma huzinunua kutokana na bei yake ya chini.