• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 1:08 PM
Msisimko duniani viongozi wakimmiminia Biden pongezi

Msisimko duniani viongozi wakimmiminia Biden pongezi

Na AFP

VIONGOZI mbalimbali duniani jana waliungana kumpongeza Rais Mteule wa Amerika Joe Biden, wengi wakieleza matumaini kwamba atarejesha umoja na ushirikiano, ambavyo vilionekana kuvurugwa na utawala wa Rais Donald Trump.

Ingawa Rais Trump alikataa kukubali matokeo hayo, viongozi wengi duniani walieleza waziwazi wanaunga mkono tangazo la ushindi wa Biden na mgombea-mwenza Kamala Harris.

“Heko! Nawatakia kila la heri kutoka moyoni mwangu. Urafiki na ushirikiano wetu unapaswa kuendelea kuwa thabiti ikiwa tunataka kuepuka changamoto zinazotukabili kwa sasa,” akasema Chansela Angela Merkel wa Ujerumani, kwenye taarifa iliyotolewa na msemaji wa serikali yake.

Rais Emmanuel Macron alisema: Raia wa Amerika wamemchagua Rais. Heko Biden na Kamala Harris! Tuna mengi ya kufanya kuepuka changamoto zinazotukabili. Tufanye kazi pamoja!”? Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson pia alimpongeza Biden kwa ushindi huo.

“Amerika ndiye mshirika wetu wa karibu zaidi. Natarajia kushirikiana nayo katika masuala yanayotuathiri pamoja kama biashara, mabadiliko ya hali ya hewa na usalama,” akasema Johnson.

Waziri Mkuu wa Ireland, Michael Martin, alikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kumpongeza Biden kwa kusema: “Ningetaka kumpongeza Rais Mpya Mteule Joe Biden. Amekuwa rafiki wa karibu wa taifa hili kwa muda mrefu. Natarajia kushirikiana naye miaka ijayo. Vile vile, natarajia kumkaribisha nyumbani.”

Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis alisema: “Heko Rais Mteule Joe Biden. Umekuwa rafiki wa kweli wa Ugiriki. Ni matumaini yangu ushirikiano kati ya nchi yetu utaendelea kukua chini ya uongozi wake.”

Waziri Mkuu wa Italia Guiseppe Conte alisema: “Tuko tayari kufanya kazi pamoja na Rais Mteule Joe Biden kukuza uchumi na biashara kati ya nchi zetu. Italia inaihakikishia Amerika kuwa mshirika wa kweli.”Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri alisema anatarajia kuimarisha uhusiano wa taifa hilo na Amerika chini ya uongozi wa Biden.Hata hivyo, Rais Andres Manuel Lopez wa Mexico, alisema ni mapema sana kumpongeza Biden hadi pale michakato yote ya kisheria itakapokamilika.

“Hatutaki kuonekana kama watuwasiojali. Lazima tuheshimu haki za watu kujieleza,” akasema Lopez, ambaye ni miongoni mwa viongozi wachache waliokuwa na uhusiano mzuri na Trump.

Vyombo mbalimbali vya habari duniani, yakiwemo magazeti pia vilmpongeza Biden kwa kuandika jumbe za kumtakia heri kwenye utawala wake.Hata hivyo, vilimwonya dhidi ya changamoto nyingi zinazomngoja katika kurejesha umoja nchini humo.

Vile vile, vilimwangazia pakubwa Harris, ambaye anatarajiwa kuwa makamu wa rais wa kwanza mwanamke Mweusi.“Mapambazuko Mapya kwa Amerika” likaandika gazeti la ‘The Independent’ nchini Uingereza.

Gazeti pia liliweka picha kubwa ya wawili hao katika ukurasa wake wa kwanza. Gazeti la ‘Sunday Times’ liliweka picha iliyosherehekea mchango wa wanawake Weusi nchini Amerika.

Liliandika kwenye ukurasa wake wa kwanza: ‘Joe Aiamsha Amerika.’Trump amekuwa akimtaja Biden kuwa “kiongozi anayesinzia.”Gazeti la ‘Sunday People’ liliandika: ‘Mungu Aibariki Amerika.’

Gazeti maarufu la ‘Bild’ nchini Ujerumani liliweka picha ya Trump kwenye ukurasa wa kwanza na ujumbe: ‘Kuondoka bila hekima.’Gazeti la Suddeutsche Zeitung pia la Ujerumani liliandika: ‘Ukombozi na Afueni Kubwa!’

Hata hivyo, lilieleza kwamba Biden anachukua mzigo mkubwa, kinyume na watangulizi wake.Nchini Australia, gazeti la ‘Daily Telegraph’ linalomilikiwa na bwanyenye Rupert Murdoch liliangazia hatua ya Trump kutokubali matokeo hayo, likimtaja kuwa “chemichemi ya hasira.”

“Kuna uwezekano (Trump) hatakubali matokeo hayo, hasa ikizingatiwa alishindwa na mpinzani aliyempuuza sana,” likaeleza.Nchini Brazil, vyombo vya habari vilifananisha kushindwa kwa Trump na hali inayomngoja rais wa taifa hilo, Jair Bolsonaro, ambaye amekuwa akionekana kumwiga kwenye uongozi wake.

Kwa mfano, amekuwa akikataa kuheshimu maamuzi ya taasisi za kiutawala na kutotambua tafiti za kisayansi kuhusu virusi vya corona.

“Kushindwa kwa Trump ni adhabu kali kwa viongozi ambao huwa hawaheshimu taasisi za kidemokrasia. Ni funzo kuu kwa Bolsonaro,” likaandika gazeti la Folha de Sao Paulo, ambalo ni mojawapo yale yanayosomwa sana nchini humo.

“Viongozi wa Brazil wanapaswa kujifunza na matukio hilo, la sivyo wasombwe na wimbi la mageuzi,” likaeleza.Ushindi wake pia ulisifiwa na vyombo mbalimbali barani Afrika.

You can share this post!

Mamlaka kuharibu bidhaa ghushi za thamani ya Sh100 milioni

Trump azidi kukaa ngumu