• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
ZULEKHA AKINYI: Mpango mzima ni kufikia upeo wa Queen Latifah katika uigizaji

ZULEKHA AKINYI: Mpango mzima ni kufikia upeo wa Queen Latifah katika uigizaji

NA JOHN KIMWERE, NAIROBI

‘MTAKA cha mvunguni sharti ainame.’ Ndivyo wahenga walivyosema na tangia zama hizo ndivyo ilivyo hadi sasa. Ni msemo ambao kwa muda unaendelea kuonekana una mashiko sio haba miongoni mwa jamii.

Pia unaonekana unaendelea kudhihirishwa na kina dada wengi tu hasa wale wameamua kujituma kisabuni kwenye masuala mbali mbali katika harakati za kujitafutia riziki.

Kati yao ni mwigizaji na mchekeshaji Zulekha Akinyi Otieno maarufu kama Zulekha Walalo Ajaab ambaye sura na sauti yake sio geni kwa wapenzi wa burudani. Mama huyu ambaye amebarikiwa watoto wanne ni mwigizaji, mcheshi, mtangazaji na mwanabiashara anayejivunia kuwa na uwezo wa kuzungumza lugha tofauti maana amezaliwa na wazazi kutoka jamii mbili tofauti-Msomali na Luo.

Wengi wanamkumbuka alipokuwa mtangazaji wa kipindi cha Maisha Jioni kilichokuwa kinapeperushwa kupitia stesheni ya Redio Maisha pia Qwetu Redio katika kipindi cha Mid Morning Show.

Zulekha anajivunia kuzoa tuzo kadhaa katika masuala ya uigizaji na ucheshi. ”Nilianza kujituma katika uigizaji mwaka 2010 kutokana na msukumo wa mitihani ya maisha baada ya kujikuta nikitapatapa kwa kushindwa kugharamia mahitaji yangu muhimu,” alisema na kuongeza kwamba mwanadamu anapojikuta kwenye wakati mgumu anastahili kufahamu kuwa Mungu ana sababu ya kumletea hali hiyo.

Mwana dada huyu anasema katika tasnia ya uigizaji analenga kufikia hadhi ya waigizaji mahiri duniani kama Dana Elaine Owens mzawa wa Marekani maarufu Queen Latifah. Kando na uigizaji Dana ni mwimbaji, mwandishi wa nyimbo, rapa pia produsa anayejivunia kuigiza filamu kama ‘Last Holiday,’ ‘Girls Trip,’ ‘Set it off,’ ‘Beauty Shop,’ ‘Just Wright,’ na ‘Hairspray,’ kati ya zingine.

”Bila kuongezea kachumbari msanii huyo ana kipawa cha uigizaji pia ni mwanabiashara hodari,” akasema na kuongeza kuwa anatamani sana kuibuka mwigizaji mkubwa hapa nchini.

Zulekha anajivunia kuigizaji vipindi mbali mbali zilizopata mpenyo kupeperushwa kupitia runinga tofauti kama NTV, KTN, Citizen, K24 na Maisha Magic. Dada ameshiriki kipindi kama ‘Vioja mahakamani,’ ‘Churchill,’ ‘Mshamba,’ na ‘Inspekya Mwala,’ kati ya zingine.

Anasema ndani ya miaka mitano ijayo analenga kuwa na brandi yake pia chuo cha kufunza masuala ya filamu. ”Katika mpango mzima ninatamani sana kukuza wasichana wanaokuja katika sekta hii maana wengi wao huwa vigumu kupata nafasi kwa sababu ya timu mafisi. Wanadada wengi hukosa kupata nafasi kuonyesha ujuzi wao ambapo hunyimwa ajira na baadhi ya maprodusa kwa sababu za ovyo tu,” akasema.

Anashauri wasichana wasome maana bila masomo maisha ya siku hizi siyo rahisi. Pia anawataka waheshimu mili yao wala wasikubali kushushwa hadhi na maprodusa wa kiume ambao hupenda kuwa na mahusiano ya kimapenzi nao kisa kuwasaidia kupata ajira.

You can share this post!

Vibarua wakana kuiba kalamu na karatasi KICC

TERESIA NJOKI: Ubunifu ni muhimu katika uigizaji