• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
Mihadarati ya Sh70,000 yanaswa Nakuru

Mihadarati ya Sh70,000 yanaswa Nakuru

NA RICHARD MAOSI

Polisi katika Kaunti ya Nakuru wamekamata vijana wanaodaiwa kuwa kundi haramu kwa jina Confirm, ambalo limekuwa likiwahangaisha wakazi.

Vijana hao tisa walikamatwa na dawa za kulevya ya kima cha Sh70,000 pamoja na simu mbili, baada ya polisi kuendesha operesheni katika eneo la Kaloleni mtaa wa Bondeni.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, kamanda wa polisi wa Nakuru Mashariki Bi Elena Kabukuru, aliwaomba wazazi kuchukua jukumu la kuwashauri vyema watoto wao wakati huu wa likizo ndefu.

Baadhi yao wanadaiwa kupoteza mwelekeo wa maisha na kuingilia starehe na anasa, jambo ambalo linalochangia kupata mimba za mapema.

Aidha alisema maeneo ya Bondeni na Kivumbini yamekuwa yakitumika kama maficho kwa magenge, yanayohusisha wavulana na wasichana.

Kabukuru aliwaomba vijana kutafuta kazi za kufanya badala ya kutumia njia ya mkato kupata hela.

Isitoshe alitoa onyo kali kwa wale wanaosambaza mihadarati kwa wanafunzi wa shule, akidai kuwa watakabiliwa na polisi na kufikishwa mahakamani.

“Hii ni onyo kwa makundi ambayo yanawasambazia vijana mihadarati.Wafahamu kuwa serikali inaendelea kuwasaka na hivi karibuni watatiwa nguvuni,”akasema.

Kuanzia siku ya Jumatatu usiku polisi wamekuwa wakishika doria katika mitaa ya mabanda, viungani mwa mji wa Nakuru kukabiliana na magenge haramu, ambayo yanaendelea kushika kasi, hususan wakati huu ambapo vijana wengi hawana kazi.

Vijana hao wamezuiliwa katika kituo cha polisi cha Bondeniwakisubiri kufikishwa mahakamani.

Mitaa ya Bondeni, Kivumbini, Free Area , Lakeview na Flamingo imekuwa ikiripoti visa vingi vya uhalifu, huku raia wakilaumu serikali kwa kusalimu amri wakati wa kukabiliana na uhalifu.

You can share this post!

Bunge kuzindua kanuni zake katika Kiswahili leo

Je, chama cha wilibaro kitasajiliwa?