• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
NHIF haitagharamia matibabu ya corona – Serikali

NHIF haitagharamia matibabu ya corona – Serikali

Na CHARLES WASONGA

WAKENYA masikini wanaougua Covid-19 na wamejisajili kwa Hazina ya Bima ya Kitaifa ya Matibabu (NHIF) wataendelea kugharamia matatibu yao kwa sababu hazina hiyo hitalipia bili zao.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na Afisa Mkuu Mtendaji wa NHIF Peter Kamunyo walisema hatua hiyo itakuwa ghali kiasi kwamba hazina hiyo haitaweza kumudu. Kampuni za kibinafsi za bima pia hazitaweza kumudu gharama hiyo.

“Haiwezekani kwa NHIF na kampuni za kibinafsi za bima kugharamia majanga kwani ni kinyume cha sheria na taratibu zinazoongoza sekta ya bima,” akaambia wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wao Michael Mbito (Seneta wa Trans Nzoia).

Hata hivyo, waziri Kagwe alisema serikali imeingilia kati na kupunguza gharama au kufutilia mbali bili za matibabu kwa Wakenya masikini ambao hawawezi kumudu malipo hayo.

Alisema hayo alipofika mbele ya Kamati hiyo, kwa njia ya mtandao, kujibu malalamishi ya maseneta kwamba NHIF na kampuni za kibinafsi za bima zimedinda kugharamia matibabu ya wanachama wao waliathirika na Covid-19.

“Malipo ya magonjwa yalitangazwa kuwa majanga ulimwenguni kama vile Covid-19 yanaweza tu kufadhiliwa na asasi za nje ambazo zitapitisha fedha hizo kwa hospitali fulani zilizoidhinishwa a serikali,” Bw Kagwe akaeleza.

Wakenya wengi wamewasilisha malalamishi yao kwa maseneta na wabunge kwamba wanalazimika kubeba mzigo mzito wa gharama ya matibabu yao licha ya kwamba wao kuwa wanachama wa NHIF na wamekuwa wakiwasilisha michango ya kila mwezi bila kuchelewa.

“Masaibu kama hayo yamekuwa wakiwakumba wale waliochukua bima ya afya kupitia kampuni za bima za kibinafsi. Hili ni suala nyeti kabisa kwa sababu baadhi ya wagonjwa wamefungiwa katika wadi hata baada ya kupona kwa kushindwa kulipa bili,” akasema Seneta wa Narok Ledama Ole Kina.

You can share this post!

Anafuata ndoto zake licha ya kutengwa na mama yake tangu...

Wanasoka 7 waliotemwa na Liverpool na wakaishia kuwa...