Java yawaomba wafanyakazi wajiuzulu kwa hiari
NA WANGU KANURI
Mkahawa wa Java wenye afisi zake kuu jijini Nairobi umewapa wafanyikazi wake notisi ya kujiuzulu kwa hiari kabla ya wiki mbili kutamatika. Fomu za kujiuzulu zitakuwepo tayari kwa wafanyikazi hapo Novemba 27, 2020.
Kupitia ilani ambayo iliandikiwa wafanyikazi hao, hoteli hiyo ilisema kuwa hata baada ya vikwazo walivyoweka kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19, mauzo yao yamedidimia ikilinganishwa na mwaka jana.
Imesema kuwa kwa wale ambao watajiuzulu kwa hiari yao watapewa marupurupu yao. Mpango huo utakuwa kwa kila tawi la mkahawa huo haswa kwa wafanyikazi ambao wamefanya kazi kwa miaka minne, wafanyikazi ambao hulipwa kutokana na mauzo na wafanyikazi ambao wamefanya kazi kwa miaka mitatu pamoja na wapishi, wanaboda boda, wahudumu na mabawabu ambao wamefanya kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu.
Vile vile wafanyikazi hao watapokea mshahara wa siku 15 kwa kila mwaka waliofanya kazi na nyongeza ya mshahara wa mwezi mmoja na nusu ili kufidia siku ambazo hawaendi kazini.
Mkahawa huo wa Java ambao una mikahawa 80 katika nchi zilizoko Afrika Mashariki, umetatizika sana tangu corona ilipobisha. Mnamo Aprili, mkahawa huo uliwakata wafanyikazi mshahara kwa asilimia 40 ili kushughulikia matakwa yaliyowekwa na serikali kwa mahoteli.
Kuwepo kwa kafyu nchini kumetatiza saa ambazo hoteli hufungwa kwa kawaida na hilo likapunguza faida.